Hizbullah yaanzisha mashambulizi makubwa ndani ya Israel, yalenga shabaha muhimu
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kuwa imeanzisha mashambulizi ya anga yanayoshirikisha idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani (drone) kuelekea eneo la ndani la Israel.
Taarifa iliyotolewa na Hizbullah imesema, mashambulizi hayo ya anga yameanza kwa kulenga shabaha maalumu ya kijeshi ya Israeli ambayo itatangazwa baadaye na kuongeza kwamba, shambulio hilo linakuja ndani ya mfumo wa "jibu la awali kwa mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Kamanda Fuad Shukr.
Harakati hiyo imesema kuwa operesheni yake mpya imeanza "kwa shambulio la anga la idadi kubwa ya ndege zisizo na rubani kuelekea ndani ya ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni (Israel) na kulenga shabaha maalumu ya kijeshi ambayo itatangazwa baadaye."
Imesisitiza kwamba, sambamba na haya, "idadi ya maeneo ya adui, kambi na maeneo ya Iron Dome kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu vimelengwa kwa idadi kubwa ya makombora," na kwamba operesheni yake itachukua muda, na baada ya hapo itatoa taarifa kamili kuhusu mwenendo na malengo yao.
Ripoti zinasema kuwa timu ya wizara ya usalama huko Israel imetakiwa kufanya mkutano wa dharura mapema leo asubuhi kutokana na hujuma huyo ya Hizullah ya kulipiza kisasi cha kamanda wake.
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon iimesisitiza kuwa, iwapo raia wa Lebanon watadhurika "adui Mzayuni" itapewa adhabu kali na iumizayo.