Majibu ya Hizbullah ya Lebanon kwa mauaji ya "Fuad Shukr"
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i115660-majibu_ya_hizbullah_ya_lebanon_kwa_mauaji_ya_fuad_shukr
Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetekeleza kwa mafanikio hatua ya kwanza ya kulipiza kisasi cha mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Fuad Shukr, aliyekuwa mmoja wa makamanda wakuu wa harakati hiyo, licha ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kujitayarisha kwa muda mrefu kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi hayp.
(last modified 2024-08-26T07:06:16+00:00 )
Aug 26, 2024 07:06 UTC
  • Sayyid Hassan Nasrullah
    Sayyid Hassan Nasrullah

Harakati ya Hizbullah ya Lebanon imetekeleza kwa mafanikio hatua ya kwanza ya kulipiza kisasi cha mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Fuad Shukr, aliyekuwa mmoja wa makamanda wakuu wa harakati hiyo, licha ya jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kujitayarisha kwa muda mrefu kwa ajili ya kukabiliana na mashambulizi hayp.

Katika taarifa yake ya kwanza, Hizbullah ilitangaza kwamba: Alfajiri ya Arubaini ya Imam Hussein, Kinara wa Mashahidi na dhihirisho la kujitoa mhaga, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake, na katika muktadha wa jibu la awali dhidi ya shambulizi la kikatili la utawala wa Kizayuni katika viunga vya kusini mwa Beirut, ambalo lilipelekea kuuawa shahidi Fuad Shukr na idadi kadhaa ya raia wa nchi hiyo, wapiganaji wa Muqawama wa Kiislamu wamelenga vituo, maeneo, kambi za kijeshi na mfumo wa ulinzi wa anga (Irone Dome) wa adui Mzayuni kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu kwa kutumia idadi kubwa ya makombora na kupiga shabaha maalumu ya kijeshi ya utawala huo ambayo itatangazwa baadaye.

Katika taarifa yake ya pili, Hizbullah ilitangaza kwamba: Hatua ya kwanza ya kulipiza kisasi imetimia kwa mafanikio kamili, na hatua hii imelenga kambi za jeshi na maeneo ya Israel ili kuondoa vizuizi vya makombora na ndege zisizo na rubani na baadaye kulenga shabaha maeneo ya ndani zaidi, kwa kurusha makombora 320 katika vituo 11 vya kijeshi, kiintelejensia na kiusalama vya utawala wa Kizayuni.

Hizbullah yashambulia maeneo nyeti ya Israel

Hizbullah imetangaza katika taarifa yake ya tatu kwamba: Ndege zote zisizo na rubani zilielekea kwenye shabaha zilizokusudiwa kwa wakati uliopangwa na kulenga shabaha kwa mafanikio. 

Wataalamu wanaamini kuwa, operesheni halisi ya shambulizi hilo la Hizbullah ya kujibu mauaji yaliyofanywa na Israel dhidi ya Shahidi Shukr ilikuwa ile ya ndege zisizo na rubani (drones) ambazo zililenga shabaha muhimu ya kijeshi, na kwamba makombora 320 yaliyorushwa yalilenga kushughulisha mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel, Iron Dome. Ripoti za karibuni zinaonyesha kuwa, kwa mara ya kwanza kabisa, Hizbullah imetumia kombora la balestiki ambalo lililenga shabaha bila kizuizi chochote. Kwa kutegemea habari za kuaminika, Televisheni ya Al-Mayadeen imeripoti kuwa, hatua ya kwanza ya operesheni ya Hizbullah ya Lebanon ya kulipiza kisasi cha mauaji ya shahidi Fuad Shukr imefanikiwa kikamilifu na ilitekelezwa kwa usahihi na umakini wa hali ya juu.

Kufuatia mashambulizi makubwa ya makombora ya Hizbullah ya Lebanon kaskazini mwa ardhi zinazokaliwa kwa mabavu za Palestina, Yoav Gallant, Waziri wa Vita wa Israel ametangaza "hali ya hatari" kwa muda wa saa 48, kuanzia saa 6:00 asubuhi ya jana. Fukwe zote za Haifa zimefungwa kwa Waisraeli kutokana na hali ya usalama. Vyuo vikuu vya Israel pia vimesitisha mitihani na shughuli zao zote. Wazayuni waishio katika vitongoji vya walowezi huko Tiberias na Haifa na vitongoji vya walowezi wa kaskazini mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu karibu na mpaka wa kusini mwa Lebanon wametakiwa kubakia kwenye mahandaki na maficho ya chini ya ardhi. 

Wazayuni wameingia na kiwewe kwa mashambulizi ya Muqawama

Ingawa utawala ghasibu wa Israel daima uko katika hali ya tahadhari, na ndege zake za kivita zinaruka juu ya anga ya Lebanon kila usiku, lakini haukuweza kuzuia makombora na drones za Hizbullah kupiga shabaha zilizokusudiwa. Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni vimekosoa utendaji wa jeshi la utawala huo katika kukabiliana na mashambulizi ya makombora ya Hizbullah na kutangaza kuwa, tangu asubuhi ya jana tumesikia madai kwamba, jeshi limefanikiwa kuzuia makombora kupiga maeneo ya Ben-Gurion na Tel Aviv, lakini hakuna maelezo yoyote kuhusu takriban makombora 320 na makumi ya ndege zisizo na rubani ambazo zilishambulia kaskazini mwa Israel. Vyombo hivyo vya habari vimekiri kwamba, moto wa hatua ya kwanza ya majibu ya Hizbullah ulitanda eneo la kilomita mraba 1,500 kaskazini mwa Israel na kwamba Hizbullah ilipanga kurusha takriban makombora na drones 6,000 dhidi ya Israel.

Kwa utaratibu huo, tunaweza kusema kwamba, sambamba na kushindwa mazungumzo ya Doha, Netanyahu amepokea hatua ya kwanza ya majibu ya Hizbullah kwa mauaji ya Fuad Shukr, ambayo yalichelewa kidogo; na kwa kuzingatia kwamba mauaji ya Shukr yalifanyika siku moja kabla ya mauaji ya Ismail Haniyeh mjini Tehran, hofu ya Wazayuni imeongezeka maradufu kutokana na ukweli kwamba, jibu la Hizbullah katika awamu hii ya kwanza, ni utangulizi wa majibu yanayofuata kutoka kwa mhimili wa Muqawama.

Ingawa hatua ya kwanza ya jibu la Hizbullah kwa mauaji ya Israel dhidi ya Shukr ilikuwa kubwa na kali, lakini wakati huo huo ilikuwa ya kiungwana; na tofauti na utawala wa Kizayuni ambao hautofautishi baina ya shabaha za kijeshi na za kiraia, Hizbullah imelenga kikamilifu shabaha za kijeshi, jambo ambalo linaongeza maradufu thamani ya operesheni ya kijeshi ya Hizbullah. Kwa nini? Kwa sababu hatua hiyo inaonyesha kwamba, Hizbullah inafanya kazi kama jeshi la kitaaluma na ina uwezo na kupata taarifa zote zinazohitajika kwa ajili ya kupata ushindi wa kimkakati.