Sep 12, 2024 07:40 UTC
  • Sinwar: Kuuawa shahidi Haniya kutaongeza uthabiti wetu hadi tuifute Israel katika ardhi yetu

Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS, Yahya Sinwar amesema kuuawa shahidi mtangulizi wake Ismail Haniya na wapiganaji wengine wa Palestina kutaongeza nguvu ya Muqawama katika mapambano yake ya kuutokomeza utawala bandia wa Kizayuni wa Israel.

Sinwar ameyasema hayo katika salamu zilizotumwa kwa viongozi mbalimbali wa Kiislamu, ambao walikuwa wametuma salamu za rambirambi kwa harakati hiyo kufuatia kuuawa shahidi Haniya.
 
Kiongozi huyo wa zamani wa Hamas aliuawa shahidi mwishoni mwa mwezi Julai katika shambulio la kigaidi lililotokea katika mji mkuu wa Iran Tehran, ambako alikuwa amekuja kuhudhuria sherehe za kuapishwa Rais mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Masoud Pezeshkian.

Katika salamu zake hizo, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Hamas amesema: "damu hii safi na misafara iliyobarikiwa ya mashahidi itaongeza tu uimara na nguvu zetu katika kukabiliana na utawala wa Kizayuni wa Kinazi hadi utakapotimuliwa na kufutwa kabisa katika ardhi yetu na matakatifu yetu".

Yahya Sinwar

Sinwar ameendelea kueleza kwamba, ushindi huo kamilii utafuatiwa na Wapalestina kuanzisha nchi yao huru yenye mamlaka kamili na mji mtakatifu unaokaliwa kwa mabavu wa al-Quds ukiwa ndio mji mkuu wake.

Katika sehemu nyingine ya salamu zake hizo, Yahya Sinwar amesema, kifo cha Haniya kimethibitisha kwamba damu ya viongozi wa Muqawama na wapiganaji wake si yenye thamani zaidi kuliko damu ya Wapalestina wengine.

Aidha, ameahidi kushikamana na njia iliyofuatwa na Shahidi Ismail Haniya, muhimu zaidi likiwa ni la kuwaunganisha Wapalestina na kuwafanya wawe kitu kimoja katika kushikamana na chaguo la Jihadi na Muqawama na kuepusha migawanyiko na mifarakano.../