Azma ya Iran na Iraq ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na viongozi wa Iraq wamesisitiza nia na azma ya serikali za Tehran na Baghdad kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wa pande mbili na ushirikiano wa kieneo.
Jumatano asubuhi Rais Pezeshkian alisafiri kwenda Iraqi katika safari yake ya kwanza nje ya nchi akiwa rais wa Iran ambapo ameongoza katika safari hiyo ujumbe wa ngazi za juu wa viongozi wa kisiasa na kiuchumi wa nchi yake. Pezeshkian ambaye alilakiwa rasmi na Waziri Mkuu wa Iraq baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad, amefanya mazungumzo katika vikao tofauti na Rais, Waziri Mkuu na Mkuu wa Baraza Kuu la Mahakama za Iraq.
Masuala ya pande mbili na ya kikanda yamejadiliwa katika vikao hivyo na viongozi wa Iraq. Kuhusu masuala ya pande mbili, viongozi wa nchi mbili wamesisitiza haja ya kufuatiliwa makubaliano ya zamani na kukuza uhusiano katika nyanja tofauti, haswa katika sekta ya uchumi. Mbali na hayo Rais Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mohammad Shia as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq, wameshuhudia kutiwa saini hati 14 za ushirikiano na maelewano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kibiashara, kiutamaduni na kijamii. Pezeshkian amesema hati hizo 14 za ushirikiano kati ya Iran na Iraq zimetiwa saini ikiwa ni mwanzo wa upanuzi wa ushirikiano wa Iran na Iraq.
Hivi sasa, kiwango cha biashara kati ya nchi mbili hizi jirani ni karibu dola bilioni 12. Mohammed Kazem Al-Sadegh, Balozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran nchini Iraq, amesema kuhusiana na suala hilo katika kikao cha Rais na wafanyabiashara na wanaojishughulisha na masuala ya kiuchumi huko Iraq kwamba nchi hiyo ni mshirika muhimu wa kibiashara wa Iran na kwamba kiwango cha biashara kati ya nchi hizi jirani ni cha thamani ya dola bilioni 12, ambapo karibu asilimia 20 yake inatokana na mauzo ya mafuta ya Iran kwa Iraq. Samad Hassanzadeh, mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wa Iran, pia amesema katika kikao hicho kwamba uwezo wa Iraq kupokea bidhaa za Iran ni mkubwa zaidi kuliko mauazo ya hivi sasa kwa nchi hiyo. Ameongeza kuwa kiwango cha hivi sasa cha mabadilisho ya biashara kati ya nchi mbili kinaweza kuongezwa kirahisi hadi kufikia dola bilioni 20 kwa mwaka.
Moja ya vikwazo muhimu katika kustawishwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Iran na Iraq ni vikwazo vya kidhalimu vya Marekani. Vikwazo hivi vimebana pakubwa uwezo wa nchi mbili katika kubadilishana bidhaa na miamala ya kibiashara licha ya irada na azma kubwa ya viongozi wa Iraq ya kustawisha uhusiano wa kiuchumi na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Kwa msingi huo, Masoud Pezeshkian, licha ya kukiri kuwepo matatizo yanayosababishwa na vikwazo hivyo katika njia ya maendeleo ya kiuchumi na kibiashara na uwekezaji kati ya nchi mbili, amesisitiza haja ya kuundwa majopo maalum ya kazi kwa ajili ya kubuni mipango ya muda mrefu ya kutatua vikwazo na kuendeleza biashara, mabadilishano ya kiuchumi na uwekezaji kati ya nchi mbili za Iran na Iraq.
Mbali na nyanja ya kiuchumi, pande hizo pia zimejadili masuala ya kiusalama. Kuwepo kwa baadhi ya makundi ya kigaidi katika maeneo ya kaskazini mwa Iraq na pia uwekezaji wa utawala wa Kizayuni huko kaskazini mwa Iraq, kunahesabiwa kuwa tishio kubwa kwa usalama wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Hadi sasa Tehran na Baghdad zimeafikiana mara kadhaa juu ya udharura wa kupunguza na kuondoa kabisa vitisho hivyo, na suala hili limesisitizwa tena katika safari hii ya Pezeshkian nchini Iraq. Kuhusiana na suala hilo, Rais Pezeshkian amesisitiza kuwa kuna haja ya kutekelezwa mapatano ya ushirikiano wa kiusalama baina ya nchi mbili ili kukabiliana na magaidi na maadui, maadui ambao tokea zamani wamekuwa wakilenga uthabiti na usalama wa eneo hili. Shia as-Sudani, Waziri Mkuu wa Iraq pia amesisitiza kuwa nchi hiyo haitaruhusu upande wowote kutishia usalama wa Iran kutokea ardhi yake.
Katika mtazamo wa kikanda, matukio ya Gaza ni suala muhimu zaidi lililojadiliwa katika mazungumzo ya Pezeshkian na viongozi wa Iraqi. Pezeshkian na as-Sudani wamesisitiza ulazima wa kusitishwa mara moja mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza. Katika kikao na Waziri Mkuu wa Iraq, Pezeshkian amesema matukio hayo yamefichua sura halisi ya utawala katili wa Kizayuni unaofanya mauaji ya kimbari pamoja na ya serikali zinazouunga mkono utawala huo zinaodai kutetea haki za binadamu. Jinai za utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza zimethibitisha wazi uwongo wa madai ya nchi za Magharibi na mashirika ya kimataifa kuhusu suala zima la haki za binadamu.