Onyo kali la Baghdad dhidi ya hatua ya Israel ya kumvunjia heshima Ayatullah Sistani
(last modified Thu, 10 Oct 2024 12:13:45 GMT )
Oct 10, 2024 12:13 UTC
  • Onyo kali la Baghdad dhidi ya hatua ya Israel ya kumvunjia heshima Ayatullah Sistani

Serikali ya Iraq imelaani vikali ufidhuli na hatua ya utawala wa Kizayuni wa Israel ya kumuweka kiongozi wa juu zaidi ya Kiislamu nchini Iraq, Ayatullah Ali al-Sistani, kama mmoja wa walengwa wa mipango ya mauaji ya kigaidi ya Israel.

Taarifa ya serikali ya Iraq imeitaka jamii ya kimataifa kulaani njama zinazofanywa za kuwashambulia watu wenye ushawishina  wenye hadhi ya kimataifa.

Basim al-Awadi, msemaji wa serikali ya Iraq amesema kuwa, baada ya utawala wa Kizayuni kuingia katika vita vya mauaji ya kimbari na kufanya jinai za waziwazi dhidi ya binadamu na kuanza mauaji na mapigano waziwazi huko Gaza na Lebanon, sasa ni zamu ya vyombo vya habari vya kibaguzi kufanya jaribio la kukashifu na kuvunjia heshima nafasi ya Marji'iyah (uongozi wa kidini).

Ayatullah Sistani akiwa pamoja na Papa Francis, Najaf-Iraq

 

Al-Awadi amesema, serikali ya Iraq inalaani vikali hatua yoyote ile ya kutaka kutusi na kudunisha nafasi na Marjaa Sistani ambaye anaheshimika na Wairaqi, ulimwengu wa Kiarabu, Kiislamu na kimataifa.

Idhaa ya 14 ya Israel imechapisha picha ya kiongozi wa juu zaidi ya Kiislamu nchini Iraq, Ayatullah Ali al-Sistani, kama mmoja wa walengwa wa mipango ya mauaji ya kigaidi ya Israel.

Picha ya Ali Sistani ilionekana pamoja na picha za kiongozi wa kundi la Ansarullah, Abdul Malik Al-Houthi, Naibu Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sheikh Naim Qassem, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) Yahya Al-Sinwar, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ismail Qaani, na Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran, Ayatullah Ali Khamenei.