Hizbullah yaendelea kuyatwanga maeneo ya Wazayuni kwa mvua ya makombora
Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon umeendelea kutoa vipigo vikali kwa walowezi wa Kizayuni kwa kuyashambulia kwa makombora maeneo ya kaskazini mwa ardhi za Palestina zilizopachikwa jina la Israel na maeneo mengine muhimu ya Wazayuni kama Haifa.
Shirika la habari la Mehr limevinukuu vyombo vya habari vya Israel vikikiri kwamba Hizbullah ya Lebanon imeendelea kuyatwanga kwa mvua ya makombora ya balestiki; maeneo mbalimbali ya utawala wa Kizayuni kama vile Kiryat Shmona na mji wa bandari wa Haifa.
Kwa mujibu wa vyombo hivyo vya Kizayuni, ving'ora vya hatari vimesikika vikilia kila kona huku mfumo wa kujilinda kwa makombora wa Israel ukishindwa kukabiliana ipasavyo na mashambulizi hayo.
Kituo cha matibabu cha Zif cha utawala wa Kizayuni nacho kilikiri jana Alkhamisi kwamba wanajeshi kadhaa wa Israel wamejeruhiwa. Tukumbuke kuwa, utawala wa Kizayuni unachuja mno habari; na duru zote za utawala huo vikiwemo vyombo vya habari vimepigwa marufuku kutangaza habari yoyote ile ambayo haikupitia kwenye mchujo mkali wa jeshi na vyombo vya usalama vya Israel.
Kwa upande wake, harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon imetangaza kwenye taarifa yake rasmi kwamba, itaendelea kuliunga mkono kwa dhati na kwa nguvu zote taifa linalodhulumiwa la Palestina hasa wakazi mashujaa na wanamuqawama wa Ukanda wa Ghaza na hakuna jinai yoyote ya Wazayuni itakayoifanya Hizbullah ibadilishe msimamo wake huo ambao inauhesabu ni jukumu lake la kidini na kibinadamu.
Hizbullah pia imetangaza kuwa imepiga kwa makombora maeneo kadhaa walikokuwa wamekusanyika wanajeshi wa utawala wa Kizayuni na kuwasababishia hasara kubwa.