'Hizbullah iko katika mkao wa vita, siku ngumu zinaisubiri Israel'
(last modified 2024-10-14T13:43:43+00:00 )
Oct 14, 2024 13:43 UTC
  • 'Hizbullah iko katika mkao wa vita, siku ngumu zinaisubiri Israel'

Kamanda Mkuu wa zamani wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ameuonya utawala haramu Israel kuhusu "siku ngumu" zijazo huku harakati ya muqawama ya Lebanon Hizbullah ikijiimarisha kivita ili kukabiliana na uvamizi wa Israel.

Meja Jenerali Mohsen Rezaei, ambaye kwa sasa ni mjumbe wa Baraza la Kuainisha Maslahi ya Mfumo Iran, ameandika katika chapisho la X siku ya Jumatatu kwamba baada ya kushuhudia wimbi la mauaji ya makamnada wake, Hizbullah sasa imeleta mabadilko katika muundo wake wa kivita.

Ameongeza kuwa: "Hivi sasa Hizbullah iko katika mkao wa kivita na hivyo siku ngumu zinawangoja Wazayuni."

Israel imekuwa ikitekeleza vitendo vya umwagaji damu vya ugaidi na uchokozi kote nchini Lebanon baada ya utawala wa Kizayuni kuanzisha vita vyake vya mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.

Takriban watu 2,306 wameuawa na wengine 10,698 wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Israel huko Lebanon tangu mapema Oktoba 2023.

Mwezi uliopita, utawala katili wa Israel ulimuua Katibu Mkuu wa Hizbullah Sayyid Hassan Nasrallah, katika shambulio la anga kusini mwa Beirut.

Tangu wakati huo, Hizbullah imeongeza mashambulizi yake ya kulipiza kisasi dhidi ya malengo ya Israel na kuahidi kuendelea na mapambano yake ya kuunga mkono Gaza na Palestina, na kuilinda Lebanon.

Siku ya Jumapili, harakati ya Hizbullah lilirusha kundi la ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya kijeshi ya Israel huko Binyamina, kusini mwa Haifa, na kuua wanajeshi wanne wa Israel na kuwajeruhi wengine 58.

 

Tags