Hamas yaonyesha silaha zake katika vita vya siku 50 na Israel
Brigedi ya Izuddin Qassam, tawi la kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeonyesha silaha zake mbalimbali ilizotumia katika vita vya siku 50 dhidi ya adui Mzayuni mwaka 2014.
Brigedi ya Izuddin Qassam imeonyesha aina mbalimbali za silaha za kisasa zikiwemo zile za kulenga shabaha,silaha maalumu kwa ajili ya wanajeshi wa nchi kavu, silaha dhidi ya vifaru na magariya deraya, makombora, maguruneti na silaha maalumu za kikosi cha wahandisi wa zana za kivita.
Wakati huo huo Brigedi ya Izuddin Qassam imewaruhusu raia wa Palestina kutembelea mojawapo ya njia za chini ya ardhi zilizokuwa zikitumiwa na wapiganaji wa harakati hiyo dhidi ya askari wa Isarel katika Ukanda wa Ghaza. Akizungumza na shirika la habari la Anatolia la Uturuki, Afisa mmoja wa Brigedi ya Izuddin Qassam amesema kuwa njia hiyo ya chini ya ardhi inatumiwa kutoa mafunzo kwa vijana na mabarobaro wa Kipalestina katika msimu wa joto.