UNRWA: Hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi yetu Ghaza
(last modified Tue, 19 Nov 2024 11:10:33 GMT )
Nov 19, 2024 11:10 UTC
  • UNRWA: Hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi yetu Ghaza

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) amesema kuwa, hakuna taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi ya shirika hilo katika kuwahudumia na kuwafikishia misaada wakazi wa Ghaza.

UNRWA ndilo shirika kubwa zaidi la misaada ya kibinadamu kwenye Ukanda wa Ghaza ambalo lilikuwa na takriban wafanyakazi 13,000 kabla ya utawala wa Kizayuni kuanzisha jinai za kutisha kwenye ukanda huo zaidi ya mwaka mmoja uliopita.

Miongoni mwa kazi za taasisi hiyo ya Umoja wa Mataifa ni kutoa misaada ya chakula na elimu kwa wananchi wa Palestina huko Ghaza na hivi sasa makadirio yanaonesha kuwa, kuna wafanyakazi 3,000 wa UNRWA wanafanya kazi kwenye eneo hilo.

Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini, amejibu maswali wa waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi kuhusu kusimamishwa kazi za shirika hilo na kusema kuwa, hakuna shirika na taasisi yoyote inayoweza kujaza nafasi ya UNRWA huko Ghaza. 

Hayo yamekuja baada ya bunge la Israel (Knesset) kutangaza siku ya Jumatatu ya tarehe 28 Oktoba, 2024 kwamba limepasisha muswada wa kupiga marufuku shughuli zote za shirika hilo la Umoja wa Mataifa.