HAMAS: Netanyahu ndiye anayewaua mateka wa Kizayuni huko Ghaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i119776
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeendelea kumlaumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kusisitiza kuwa yeye ndiye aliyefanya mauaji ya makumi ya mateka wa Kizayuni waliokuwa wanashikiliwa katika Ukanda wa Ghaza.
(last modified 2024-12-06T07:14:51+00:00 )
Dec 06, 2024 07:14 UTC
  • HAMAS: Netanyahu ndiye anayewaua mateka wa Kizayuni huko Ghaza

Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imeendelea kumlaumu Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu na kusisitiza kuwa yeye ndiye aliyefanya mauaji ya makumi ya mateka wa Kizayuni waliokuwa wanashikiliwa katika Ukanda wa Ghaza.

Hamas imesema hayo katika taarifa yake ya jana Alkhamisi na kujibu madai ya uongo ya Israel iliyodai kuwa, baada shambulio la mwezi Februari dhidi ya Khan Yunis huko kusini mwa Ghaza, huenda wapiganaji wa Muqawama waliua mateka sita wa Israel ili kulipiza kisasi.

Taarifa ya HAMAS imesema: "Netanyahu anahusika moja kwa moja na mauaji ya makumi ya mateka wa Kizayuni kutokana na kukwamisha juhudi za kusitisha mapigano. Hakuna njia mbadala isipokuwa usitishaji mapigano, kuondoka wanajeshi vamizi wa Israel kwenye Ukanda wa Ghaza na kutekelezwa makubaliano ya kubadilishana mateka."

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya HAMAS pia imebainisha kuwa, hatua ya jeshi la Israel ya kuendelea kuua mateka wa Kizayuni ni ushahidi wa kufeli njia inayotumiwa na Netanyahu ya kutaka kuwakomboa mateka hao kwa kutumia nguvu. Vile vile Hamas imeonya kuwa Waisraeli zaidi watauawa ikiwa utawala huo utaendelea kutumia njia za kijeshi kujaribu kuwakomboa kutoka mikononi mwa HAMAS.

Licha ya kupita takriban miezi 14 ya mashambulizi ya kikatili ya Israel huko Ghaza, lakini bado utawala wa Kizayuni umeshindwa kufikia malengo yake uliyotangazwa ya kuisambaratisha Hamas na kuwakomboa mateka wa Kizayuni. Ilichofanya hadi hivi sasa Israel ni ukatili wa kuwaua shahidi Wapalestina wasiopungua 44,532, wengi wao wakiwa wanawake na watoto wadogo na kuwajeruhi wengine 105,538.