Iraq kuwa makaburi ya askari wa Saudia
Vikosi vya wananchi vya Iraq maarufu kama Hashdu Shaabi vimeitahadharisha Saudi Arabia dhidi ya kuivamia nchi hiyo na kusema kuwa iwapo itathubutu kufanya hivyo, basi wataigeuza ardhi ya Iraq kuwa makaburi ya wanajeshi wa Saudia.
Ahmad al-Assadi, Msemaji wa vikosi hivyo jana Jumamosi alisema kuwa, iwapo serikali ya Riyadh itaishambulia Iraq kwa kisingizio cha kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh, basi itakabiliwa na jibu kali.
Onyo hilo la Hashdu Shaabi limekuja baada ya vyombo vya habari vya Saudia kutangaza kuwa Riyadh na waitifaki wake katika eneo hilo wanapanga kufanya luteka ya kijeshi kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu, karibu na mpaka na Iraq. Mapema wiki hii, Saudia ilisema wanajeshi wapatao laki tatu na elfu 50 kutoka mataifa ya Ghuba ya Uajemi na nchi nyinginezo zikiwemo Misri, Sudan na Pakistan zitashiriki katika mazoezi hayo ya kijeshi yaliyopewa jina la "Radi ya Kaskazini", katika eneo la Hafer al-Batin.
Msemaji wa vikosi vya wananchi vya Iraq amesema iwapo majeshi hayo yanayoshiriki luteka hiyo yatathubutu kuja karibu na mpaka wa Iraq, basi yatakabiliwa na jibu kali kutoka kwa wanajeshi wake waliojitolea kulinda mipaka ya Iraq. Wadadisi wa mambo wanasema kuwa, mazoezi hayo ya kijeshi ya Saudia ni kwa ajili ya kujiandaa kuingia kijeshi nchini Syria. Mbali na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain pia zimetangaza azma yao ya kutuma vikosi vya majeshi nchini Syria eti kupambana na kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh.