Makumi ya wafanyakazi wa UNRWA wameuawa katika vita vya Gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina UNRWA limetangaza kuwa, wafanyakazi 258 wa shirika hilo wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu kuanza kwa vita hivyo mwaka jana (2023).
Shirika la Misaada na Ajira kwa Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limesema katika taarifa yake leo kwamba, karibu mashambulizi 650 kwenye majengo na vituo vya UNRWA yamerekodiwa tangu kuanza kwa vita hivyo huku Wapalestina 745 waliokwenda kwenye vituo vya wakala huo kwa ajili ya kupata hifadhi wakiuawa shahidi wakati wa mashambulizi ya utawala wa Kizayuni.
UNRWA pia imeripoti kuwa vituo vingi vinavyoshirikiana na shirika hilo la misaada vimebomolewa au kuharibiwa.
Hapo awali, UNRWA ilikuwa imeonya kuhusu kutokea njaa katika Ukanda wa Gaza na kutoa wito wa ushirikiano wa kimataifa na kusitishwa kwa mapigano ili kutoa msaada wa kuokoa maisha katika kukabiliana na njaa inayokaribia.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) limeeleza kuwa, masaibu ya wakimbizi wa Kipalestina yanasalia kuwa mgogoro wa wakimbizi ambao haujatatuliwa kwa muda mrefu zaidi duniani, chini ya kivuli cha vita, huku jeshi la Israel likiendelea kupanua operesheni zake za kijeshi na kulipua majengo, hasa katika eneo la kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, ambalo linaendelea kuzingirwa.