Takribani misikiti 1000 imebomolewa katika vita vya Gaza
Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina imetangaza katika ripoti yake kuwa, utawala wa Kizayuni umebomea kabisa au sehemu misikiti 966 ya Ukanda wa Gaza katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita.
Ripoti ya wizara hiyo inaeleza kwamba, jeshi la Kizayuni limebomoa kikamilifu misikiti 815 ya Ukanda wa Gaza katika kipindi cha mwaka mmoja wa uchokozi na vita vya mauaji ya halaiki dhidi ya Ukanda huo.
Aidha sehemu ya misikiti isiyopungua151 imeharibiwa huku makanisa matatu pia yakiwa yamebomolewa kikamilifu.
Jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel pamoja na hujuma zake za kijeshi zimepelekea pia kubomolewa makumi ya makaburi huko Gaza.
Taarifa ya Wizara ya Wakfu ya Gaza imeendelea kubainisha kuwa, utawala ghasibu wa Israel umelenga makaburi zaidi ya 60, kufukua na kuiba miili ya mashahidi na wafu zaidi ya elfu moja.
Vilevile utawala ghasibu wa Israel umeharibu makao 15 ya Wizara ya Wakfu yakiwemo makao makuu ya wizara hiyo, makao makuu ya Radio Qur'ani, Ofisi ya usimamizi wa Wakfu huko Khan Yunis na kituo cha kuhifadhi nyaraka na kumbukumbu cha wizara hiyo; ambapo hadi sasa wafanyakazi 91 wa wizara hiyo pia wameuawa shahidi.
Aidha hujuma hizo za Israel dhidi ya Gaza zimeripotiwa kulenga ofisi za kamati za kukusanya zaka, madrasa za Qur’ani na makao makuu ya Benki ya Wakfu.
Kadhalika, mashambulizi hayo ya kinyama ya utawala wa Kizayuni yamepelekea kuuawa shahidi makumi ya wanazuoni, wahubiri, maimamu, na waadhini tangu.