Mashtaka dhidi ya askari wa Kizayuni duniani
Kufuatia kutoroka askari wa jeshi la Kizayuni kutoka Brazil na kuwasilishwa malalamiko na mashtaka mengi katika nchi zisizopungua 10 za dunia, kumewekwa mbinyo wa safari za nje za askari wa Kizayuni na shughuli zao katika mitandao ya kijamii.
Kutokana kuongezeka wasi wasi wa utawala wa Kizayuni kuhusiana na kutiwa mbaroni askari wa utawala huo katika nchi mbalimbali duniani, vyanzo vya usalama vya utawala huo vimeonya kuhusiana na suala hilo.
Redio na Televisheni za Kizayuni zimeripoti kuwa, malalamiko 50 dhidi ya askari wa utawala huu yamesajiliwa katika nchi 10 za dunia.
Gazeti la Israel la Haaretz limeripoti: "Taasisi zinazofungamana na serikali zinajiandaa kuwasaidia wanajeshi ambao wanaweza kukamatwa au kufunguliwa mashtaka wakiwa safarini nje ya nchi kwa kuhusika na uhalifu wa kivita huko Gaza. Wanajeshi hao wa Kizayuni wamearifiwa juu ya kuangalia upya uamuzi wao wa kusafiri nje ya nchi na wakati huo huo, wanapaswa kutumia kwa kiwango kidogo mitandao ya kijamii.
Kitengo cha usalama wa habari cha jeshi la Israel kinakadiria kuwa, wanajeshi huchapisha takribani maudhui milioni moja kwenye mitandao ya kijamii kila siku.
Kuhusiana na hilo, Kanali ya Al-Mayadeen ikivinukuu vyombo vya habari vya Kizayuni, iliripoti kuwa askari wanne wa utawala huo walifanyiwa uchunguzi na kupekuliwa katika nchi za Afrika Kusini, Sri Lanka, Brazil na Ufaransa kwa tuhuma za kufanya jinai za kivita.
Katika upande mwingine, mahakama moja nchini Brazil iliamuru polisi wa nchi hiyo kumchunguza mwanajeshi wa Israel aliyesafiri hadi katika nchi hiyo akituhumiwa kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza. Mwanajeshi huyu wa Israel, ambaye alikuwa amemaliza tu utumishi wake na kwenda Brazil kwa mapumziko, alikimbia kutoka nchini humo mara tu alipopata habari kuhusu uamuzi wa mahakama ya Brazil.
Tukio hili limeongeza wasiwasi katika ardhi zinazokali kwa mabavu ambazo zimepachikwa jina bandia la Israel. Yuli Edelstein, mkuu wa Kamati ya Masuala ya Kigeni na Usalama ya Bunge la Israel (Knesset), amelitaka baraza la mawaziri kuchukua hatua za kuwalinda wanajeshi wake dhidi ya mashtaka na kufuatiliwa kisheria.
Yair Lapid, kiongozi wa upinzani, pia amelishutumu baraza la mawaziri la Benjamin Netanyahu kwa kushindwa katika medani ya kimataifa na kutaka kuundwa kwa kamati ya uchunguzi ili kuzuia matukio kama hayo.
Lapid alisema: “Kulazimika mwanajeshi wa Israel kutoroka Brazil ili kuepuka kukamatwa kwa tuhuma za vita huko Gaza ni pigo la kisiasa kwa baraza la mawaziri lisilowajibika la Netanyahu."
Aidha aliongeza kuwa, “tumefikia hali ambayo Wapalestina wanafanya vizuri zaidi kuliko Israel katika anga za kimataifa na wanajeshi wetu wanakataa kusafiri kwa kuhofia kukamatwa. Kwa hakika hili ni pigo kubwa.”
Wakati huo huo, nchini Chile mwanajeshi wa Kizayuni aliyeko nchini humo amechunguzwa na mawakili 620. Hivi karibuni kundi la mawakili 620 wa Chile liliwasilisha mashtaka yao dhidi ya mwanajeshi wa Israel Sar Hirschurin kutoka Brigedi ya 749 ya Jeshi la Kizayuni, anayetuhumiwa kufanya jinai dhidi ya binadamu katika vita dhidi ya Gaza na hivi sasa yuko nchini Chile.
Nelson Haddad, mwakilishi wa kundi hilo la mawakili, katika kutoa maelezo ya malalamiko yaliyowasilishwa katika ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo la mji mkuu, alisema: "Tunaelezea kuchukizwa kwetu kwa kuweko nchini Chile afisa kutoka kitengo cha 749 cha uhandisi cha jeshi linalokalia kwa mabavu ardhi ya Palestina. Kulingana na nyaraka na ushuhuda tuliokusanya, ikiwa ni pamoja na ushuhuda wa mmoja wa wahanga na jamaa wa wahasiriwa wanaoishi katika eneo la El-Zaitun huko Gaza, mwanajeshi huyu amefanya uhalifu mkubwa.
Matukio ya kuandamwa viongozi, maafisa na wanajeshi wa Israel kutokana na kutenda jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza yamechukua mkondo na wigo mpana zaidi sambamba na kukithiri maandamano ya kulalamikia na kulaani jinai za Israel yanayoshuhudiwa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni. Hali hii imewatia kiwewe na kuwakosesha usingizi viongozi wa Israel hasa kutokana na kuongezeka himaya na uungaji mkono wa walimwengu kwa wananchi wa Palestina.
Hii ni katika hali ambayo, tayari Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) imetoa waranti wa kutiwa mbaroni Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel, Benjamin Netanyahu, na aliyekuwa waziri wake wa vita Yoav Gallant, wakituhumiwa kutenda jinai za vita.