Hamas inataka iundwe 'serikali ya makubaliano ya kitaifa' huko Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121148-hamas_inataka_iundwe_'serikali_ya_makubaliano_ya_kitaifa'_huko_gaza
Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya  Palestina ,Hamas,  amesema kundi hilo linataka iundwe serikali ya maridhiano ya kitaifa katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2026-05-19T09:45:50+00:00 )
Jan 07, 2025 23:13 UTC
  • Hamas inataka iundwe 'serikali ya makubaliano ya kitaifa' huko Gaza

Kiongozi mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu (Muqawama) ya  Palestina ,Hamas,  amesema kundi hilo linataka iundwe serikali ya maridhiano ya kitaifa katika Ukanda wa Gaza.

Osama Hamdan, mwakilishi wa Hamas nchini Lebanon na mjumbe wa ofisi ya kisiasa ya kundi hilo, aliyasema hayo katika taarifa siku ya Jumanne, wakati duru mpya ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja juu ya usitishaji vita huko Gaza ikiwa imeanza tena katika mji mkuu wa Qatar, Doha.

"Tunataka serikali ya maridhiano ya kitaifa kuwa lengo la kusimamia masuala ya Palestina katika awamu hii ya mpito hadi wananchi wa Palestina watakapoamua kuchagua uongozi wao," Hamdan alisema.

Afisa huyo wa ngazi ya juu wa Hamas amebainisha zaidi kuwa, Israel imewazingira watu wa Palestina huko Gaza na inaendelea na mauaji  ya kimbari na uharibifu na kwa msingi huo harakati ya muqawama itaendeleza njia ya mapambano na  hakuna kitakachodhoofisha azma yake hiyo.

Amesema: "Msimamo wetu wa wazi katika mazungumzo ni usitishaji vita, kuondoka jeshi vamizi la Israel, kubadilishana mateka na ujenzi wa Gaza bila masharti ya Israel."

Matamshi ya Hamdan yanakuja wakati mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yenye lengo la kutekeleza usitishaji vita huko Gaza kati ya Israel na Hamas yakiwa yameanza tena nchini Qatar.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar Majed al-Ansari alithibitisha katika taarifa yake Jumanne kwamba mikutano ya kiufundi "bado inafanyika kati ya pande zote mbili," akimaanisha mikutano na maafisa wa ngazi ya chini juu ya nukta za makubaliano.

Wapatanishi Qatar, Misri na Marekani wamekuwa katika mazungumzo ya miezi kadhaa  kati ya wawakilishi kutoka utawala wa Tel Aviv na Hamas ambayo yameshindwa kumaliza karibu miezi 15 ya vita vya Israel vya mauaji ya kimbari dhidi ya Gaza/.

Kikwazo kikuu kwa mazungumzo kimekuwa ni kusita kwa Israel kukubaliana na usitishaji wa kudumu wa mapigano.