Wabunge wa Uingereza wataka kushtakiwa Waziri Mkuu wa Israel
Wabunge wa Uingereza wametoa mwito wa kushtakiwa na kupandishwa kizimbani Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala haramu wa Israel kutokana na kutenda jinai za kivita katika Ukanda wa Gaza Palestina.
Wabunge wa Uingereza wamekosoa kuendelea mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza na kutoa mwito wa kuachiliwa huru mara moja Hussam Abu Safiya, Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Kamal Adwan katika Ukanda wa Gaza.
John McDonnell, Mbunge wa kujitegemea katika Bunge la Uingereza amekosoa vikali misimamo dhaifu ya serikali ya London kuhusiana na jinai za Israel na kusema, kukemea na kulaani tu jinai hizi za Israel pasi na kuchukuliwa hatua za kusitishwa vita ni jambo ambalo halitoshi.
Mbunge huyo wa kujitegemea wa Bunge la Uingereza amemkosoa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na maafisa wengine wa utawala huo bandia na kuongeza kuwa Israel ni utawala wa kivita unaoshambulia kwa mabomu hospitali, kuwakamata madaktari na wahudumu wa afya, kuua watoto na kuwaua wakimbizi katika maeneo ya ambayo yanatambulika kuwa ni ya amani.
Mwezi Novemba mwaka jana (2024) Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC ilitoa hati za kukamatwa waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Yoav Gallant baada ya kuwafungulia mashtaka ya kutenda jinai za kivita na jinai dhidi ya binadamu huko Gaza, ambako utawala wa Kizayuni umekuwa ukiendesha vita vya kinyama na kufanya mauaji ya kimbarii tangu mwezi wa Oktoba mwaka 2023.