Wanajeshi wa Israel wakiri kufanya uhalifu wa kivita huko Gaza
Shirika la habari la Associated Press limeripoti ushuhuda kutoka kwa wanajeshi wa Israel ambao wamekiri kufanya uhalifu wa kivita, kuwalenga watu wasio na ulinzi, na kuharibu na kupora nyumba ambazo hazikuwa tishio wakati wa ushiriki wao katika uvamizi unaoendelea kwenye Ukanda wa Gaza.
Shirika hilo limeripoti kuwa, takriban wanajeshi 200 wa Israel wametia saini barua wakisema kwamba wataacha kupigana huko Gaza kama serikali ya Waziri Mkuu, Benjamin Netanyahu, haitaafiki makubaliano ya kusitisha mapigano.
Limeeleza kuwa wanajeshi wa Israel wanaokataa kupigana huko Gaza wanasema waliona au walifanya mambo ambayo yanavuka mipaka ya maadili.
Associated Press imesema, baadhi yao wamekiri kupokea amri ya "kuchoma au kubomoa nyumba ambazo hazikuwa na tishio lolote," na kwamba wamewaona askari wenzao wakipora na kuharibu nyumba za raia wa Palestina.Gaza
Mmoja wa wanajeshi hao wa Israel amesema kuwa aliagizwa kumpiga risasi mtu yeyote aliyeingia kwenye eneo la buffer zone, na amethibitisha kuwa aliona thamani ya maisha ya binadamu ikitoweka katika kipindi hicho. Askari huyo wa Israel amesema kuwa picha ya askari wenzake wakimuua kijana wa Kipalestina ambaye hakuwa na silaha itabakia siku zote ndani ya akili yake.