Kushadidi mvutano baina ya Pakistan na Taliban kuhusu chimbuko la ugaidi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121432-kushadidi_mvutano_baina_ya_pakistan_na_taliban_kuhusu_chimbuko_la_ugaidi
Anga ya mzozo na mvutano kati ya Pakistan na kundi la wanamgambo wa Taliban linalotawala nchini Afghanistan inachukua wigo mpana zaidi.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Jan 14, 2025 23:04 UTC
  • Kushadidi mvutano baina ya Pakistan na Taliban kuhusu chimbuko la ugaidi

Anga ya mzozo na mvutano kati ya Pakistan na kundi la wanamgambo wa Taliban linalotawala nchini Afghanistan inachukua wigo mpana zaidi.

Akitegemea ripoti ya timu ya waangalizi ya Umoja wa Mataifa, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ametangaza kuwa, Afghanistan ilisalia kuwa kitovu cha uandikishaji na kuwezesha kundi la kigaidi la Daesh Khorasan mnamo 2024, na mashirika mengine kadhaa ya kigaidi, pamoja na wanachama wa Al-Qaeda na Tehreek-e-Taliban Pakistan ambao bado wanaendesha shughuli zao nchini Afghanistan.

Khawaja Muhammad Asif Waziri wa Ulinzi wa Pakistan amewashauri maafisa wa Taliban kuheshimu dhamana iliyopewa jamii ya kimataifa kwa kuharibu miundombinu ya kigaidi na kuchukua hatua zinazoweza kuthibitishwa ili kuzuia kutumiwa ardhi ya Afghanistan dhidi ya nchi nyingine.

Waziri wa Ulinzi wa Pakistan ametoa matamshi hayo kujibu msimamo wa hivi karibuni wa Sher Muhammad Stanekzai, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa serikali ya muda ya Afghanistan anayeshughulikia masuala ya kisiasa, ambaye aliona tuhuma za Islamabad dhidi ya Taliban kuwa bandia na ni jaribio la kutaka kuwaonyesha wengine kuwa ndio wakosa.

Khawaja Muhammad Asif Waziri wa Ulinzi wa Pakistan

 

Katika miezi ya hivi karibuni, mvutano katika uhusiano kati ya Pakistan na Taliban umeongezeka sana, na sababu muhimu zaidi ya hili ni matamshi ya udhalilishaji  ya maafisa wa Taliban dhidi ya Pakistan na hasira ya maafisa wa Pakistan kutokana  na Taliban kupuuza matakwa ya Islamabad.

Kundi la Taliban, ambalo linachukuliwa kuwa lilizaliwa nchini Pakistan, sasa limejitwalia sura ya uhuru na halitilii maanani ukosoaji wa Pakistan kuhusiana na uwepo wa makundi yenye silaha yanayoipinga nchi hiyo nchini Afghanistan, likiwemo kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban.

Pia, kinachoikasirisha zaidi Pakistan ni kukataliwa shutuma za Islamabad kuhusiana na kundi hilo la kigaidi na maafisa wa Taliban kuyatambua matatizo ya Pakistan kuwa ni ya ndani.

Hii ni katika hali ambayo, Pakistan inawakosoa vikali viongozi wa kundi la Taliban la Afghanistan kwa kutozingatia ahadi zao katika suala la kutoa usalama katika mipaka ya pamoja, kupambana na ugaidi na kulinda haki za wanawake na wasichana nchini Afghanistan.  Utendaji wa  kujitegemea wa Taliban na kutokubali kupewa miongozo na Pakistan imeifanya  Islamabad kuonyesha kutokuwa na nia ya kuitambua serikali ya Taliban na mara kwa mara imesema kuwa kuitambua rasmi serikali ya Taliban ya Afghanistan kunahitaji mtazamo wa kikanda na kimataifa.

Kuhusiana na hili, hivi karibuni mwakilishi wa zamani wa Pakistan nchini Afghanistan alitangaza kuwa, wanamgambo Taliban sio tu kwamba hawana uhalali na himaya ya wananchi bali wanawarushia mawe wengine ilihali wao wanaishi kwenye nyumba ya vioo, jambo ambalo linaweza kuwa onyo kubwa zaidi la Pakistani hata kuhusiana na kuwepo utawala wa Taliban nchini humo.

 

Wapiganaji wa kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban 

Muhammad Shahbaz Sharif Waziri Mkuu wa Pakistan naye ametoa matamshi ya kauli kali dhidi ya kundi la Taliban na kusisitiza kuwa, makundi ya kigaidi likiwemo Tehreek-e-Taliban Pakistan, yanaendelea kutumia ardhi ya Afghanistan dhidi ya nchi yake. Hii ina maana kwamba katika ngazi ya juu kabisa ya kisiasa ya Pakistan,  kunaendelea kushuhudiwa hali ya kutoridhika na hatua ya kutotoa ushirikiano serikali ya Taliban kuhusiana na masuala ya usalama

Mbali na mvutano huo wa maneno, shambulio la hivi karibuni la Jeshi la Pakistan katika ngome za kundi la kigaidi la Tehreek-e-Taliban nchini Afghanistan limesababisha kuibuka ufatulianaji risasi  baina ya walinzi wa mpaka wa pande zote mbili.

Kwa mtazamo wa Pakistan ni kuwa, wakati Taliban haijatambuliwa na jamii ya kimataifa, haipaswi kupuuza masuala ya usalama na kikanda na hivyo kuibuka anga ya malalamiko na hali ya kutorodhika mataifa ya kikanda dhidi yake. Kwani kwa kufanya hivyo inajipalilia kaa la moto.

Kwa sababu kundi hili linajionyesha kuwa ni mtawala ambaye hajisikii kuwajibika kwa matarajio ya nchi za kikanda kuhusu masuala ya nchi mbili, hasa usalama. Masuala ya usalama na mazingira ni changamoto za pamoja za nchi za eneo hili, na ili kukabiliana nazo ni lazima nchi zote ziwe na ushirikiano endelevu, athirifu na madhubuti.