Kuchunguzwa matokeo ya usitishaji vita Ukanda wa Gaza
Baada ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) kutangaza rasmi kukubali usitishaji vita na kuanza mchakato wa kuhitimisha vita katika ukanda huo, hapana shaka kuwa masuuala ya kimedani na kisiasa katika eneo hilo yataathiriwa na tukio hilo.
Utawala wa Kizayuni wa israel ukisaidiwa na Marekani, tangu Oktoba 7 mwaka 2023 ulianzisha vita vya uharibifu na mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza vilivyoendelea kwa zaidi ya miezi 15, na mbali ya uharibifu mkubwa wa miundombinu, vimepelekea kuuawa shahidi na kujeruhiwa maelfu ya Wapalestina ambao wengi wao ni wanawake na watoto wadogo.
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) jana Jumatano ilisema katika hatua yake ya awali baada ya kufikiwa makubaliano ya usitishaji vita Ukanda wa Gaza kwamba: Mapatano ya kusitisha vita ni matokeo ya mapambano imara ya wananchi wa Palestina na wanamuqawama shupavu wa Gaza katika kipindi za zaidi ya miezi 15 iliyopita. Hamas imeongeza kuwa: Makubaliano haya yametokana na dhima ya kuwajibika ya harakati hii mkabala wa wananchi wenye stahamala na wanamapambano ngangari ya Gaza ili kusitisha mashambulizi na vita vya adui Mzayuni kwa ajili ya kuhitimisha umwagaji damu na vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.
Watumiaji wa mtandao wa kijamii wa X pia wameanzisha hashtagi "#Gaza_Tantasir, (Gaza imeshinda) sambamba na kutangazwa rasmi habari ya makubaliano ya kusimamisha vita kati ya Hamas na Israel.
Ingawa wananchi wa Palestina wameunga mkono pakubwa tangazo rasmi la usitishaji vita na taarifa ya Hamas, lakini katika upande mwingine, katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu, Wazayuni wamekiri kushindwa na Muqawama wa Palestina na kueleza upinzani wao dhidi ya Netanyahu na baraza lake na mawaziri.
Wazayuni wenye misimamo mikali wamepinga makubaliano hayo ya kusimamisha vita na kubadilishana mateka na kusema kuwa Benjamin Netanyahu amesaini makubaliano yaliyofeli mkabala wa Hamas.
Makubaliano ya kusimamisha vita huko Gaza yataanza kutekelezwa Jumapili ya tarehe 19 mwezi huu. Masuala muhimu katika makubaliano haya ni kubadilishana mateka na kutekeleza usitishaji vita wa kudumu, na mateka wote wa kizayuni walioangamia watakabidhiwa. Mateka wa upande wa utawala wa Kizayuni ambayo walikuwa wakishikiliwa na wanamapambano wa Palestina pia watakabidhiwa kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Mkabala wa hatua hii, Israel pia imekubali kuwaachia huru Wapalestina waliopo katika jela za utawala huo. Mabadilishano ya mateka hawa na wafungwa yataanza kutekelezwa katika siku ya kusitisha vita ambayo imetajwa katika makubaliano hayo kama "siku ya kwanza".
Kwa mujibu wa makubaliao hayo, utawala wa Kizayuni na Hamas pia zimekubaliana juu ya masuala ambayo yatapelekea kufanikishwa malengo manne yaliyoainishwa, yaani kutekelezwa usitishaji vita wa kudumu, kuondoka Ukanda wa Gaza wanajeshi ghasibu wa Israel, kujengwa upya Gaza, kufunguliwa tena vivuko, kuruhusu watu kuingia na kutoka na kuwezesha usafirishaji wa bidhaa katika ukanda huo.
Makubaliano ya kusimamisha vita Ukanda wa Gaza yanatekelezwa katika hali ambayo Marekani na baadhi ya nchi za Magharibi ziliuhami na kuunga mkono pakubwa utawala wa Kizayuni kwa silaha, fedha na propaganda tangu kutekelezwa operesheni ya kimbunga cha al-Aqsa tarehe 7 Oktoba 2023. Vyombo vya habari vya Magharibi viliendesha popaganda kubwa kwa maslahi ya utawala wa Kizayuni na lengo kuu lilikuwa kunyamazisha na kuzuia kuchapishwa habari zilizofichua jinai za kutisha na mauaji ya kimbari ya Wazayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza.
Makubaliano haya ni nembo ya Muqawama na kupigania haki, na mapambano halali ya makundi ya Muqawama ya Palestina dhidi ya ukandamizaji na uvamizi wa Wazayuni.
Utawala wa Kizayuni wa Israel umeshindwa kufikia malengo na matakwa yake maovu licha ya propaganda kubwa zilizofanywa na vyombo vya habari vya nchi za Magharibi na mazingira ya kusambaratika kisiasa na kuondoka mamlakani Netanyahu yataanza baada ya kukubali kusitisha vita.
Suala jingine muhimu lililofanikiwa kutokana na muqawama wa Palestina ni kutayarishwa uwanja wa kufikishwa kwenye mahakama za kimataifa viongozi watenda jinai wa Israel kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika Ukanda wa Gaza.
Majaji huru katika maeneo yote duniani wanaweza kuwasilisha kesi mahakamani na hivyo kutayarisha mazingira ya kutiwa nguvuni na kushtakiwa Netanyahu na Yoav Gallant baada ya waranti wa kuwatia mbaroni uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) dhidi ya viongozi hao wawili wa Israel.
Makubaliano ya kusimamisha vita Gaza ni matokeo ya nguvu ya Muqawama na udhaifu wa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao haujui lolote isipokuwa kumwaga damu za watu wasio na hatia. Taathira za usitishaji vita zitazidisha hali ya mgogoro katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu (Israel) na katika upande wa pili, umoja na mshikamano utaongezeka miongoni mwa makundi ya mapambano ya ukombozi ya Palestina.