Vikwazo; Fimbo ya Magharibi katika sera ya kigeni
Wakati Marekani na nchi za Ulaya zimekuwa na nafasi kubwa katika kuwawekea mashinikizo ya kiuchumi watu wa Syria kwa kutumia vikwazo vya kikatili, sasa baada ya kuanguka utawala wa Bashar al-Assad na kushika madaraka kundi la Hay'at Tahrir al-Sham, kuna minong'ono kwamba nchi hizo zina nia ya kupunguza vikwazo dhidi ya nchi hiyo.
Nchi sita, yaani Ujerumani, Ufaransa, Uholanzi, Uhispania, Finland na Denmark, zimependekeza kufanyiwa marekebisho muundo wa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Syria, kwa sharti kwamba Damascus iahidi kuheshimu haki za binadamu na haki za waliowachache. Pendekezo hili la nchi sita wanachama wa EU linasisitiza kufunguliwa njia za kifedha kati ya Umoja wa Ulaya na Syria.
Zaidi ya mwezi mmoja umepita tangu kuporomoka kwa mfumo wa kisiasa wa Syria na kupinduliwa utawala wa Bashar al-Assad. Moja ya sababu kuu za kuanguka Bashar al-Assad kutoka madarakani ni mgogoro wa kiuchumi uliokuwepo nchini Syria. Mgogoro huo umesababisha mashinikizo makubwa ya kiuchumi kwa watu wa Syria. Mashinikizo hayo ya kiuchumi yalikuwa makubwa sana kiasi kwamba wastani wa mshahara wa wafanyikazi ulikuwa dola 20, wakati mfumuko wa bei ulikuwa kwa uchache mara 10 ya wastani wa mshahara.
Kumetajwa sababu nyingi za mgogoro wa kiuchumi wa Syria, lakini hapana shaka kuwa vikwazo vya kidhalimu vilikuwa mojawapo ya sababu muhimu zaidi. Marekani imekuwa ikitekeleza vikwazo vya Caesar Act dhidi ya Syria tangu mwaka 2020. Vikwazo hivyo vimekuwa kizingiti kikubwa kwa uwekezaji na uzalishaji wowote wa mapato ya serikali ya Syria. Vikwazo hivyo vilizizuia hata nchi za Kiarabu uwekeza nchini Syria. Matokeo yake, mgogoro wa kiuchumi ulizidi kuwa mbaya kila mwaka na hatimaye ulipelekea kupinduliwa utawala wa Bashar al-Assad na kuondolewa madarakani.
Sasa, baada ya kupinduliwa utawala wa Bashar al-Assad, nchi za Ulaya zimetaka kufanyike marekebisho katika muundo wa vikwazo dhidi ya nchi hiyo. Kuhusiana na hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock, ameahidi kupunguzwa vikwazo vya Umoja wa Ulaya kutokana na kupinduliwa serikali ya Bashar al-Assad. Akitetea uamuzi wake huo kando ya kongamano la kimataifa huko Riyadh, afisa huyo wa Ujerumani amesema: "Kama jamii ya kimataifa, hatupaswi kuruhusu kutoweka fursa ya mustakbali wa Syria. Ndio maana sisi, kama Ujerumani na Ulaya, tunachukua hatua madhubuti za kwanza katika mwelekeo huu."
Matamshi haya yanaonesha kuwa, nchi za Magharibi zinapoipinga serikali ya nchi fulani, haki za binadamu huwa hazina maana tena kwao na zinatoa mashinikizo makubwa zaidi kwa raia wa nchi hiyo katika sura ya vikwazo vya kikatili. Mwenendo huo wa vikwazo ulitekelezwa dhidi ya Syria. Sasa, wakati kundi la Tahrir al-Sham likiwa bado kwenye orodha ya ugaidi, nchi za Magharibi zinazungumzia suala la kufanyia marekebisho muundo wa vikwazo. Sababu ya suala hilo ni kuwa, harakati ya Tahrir al-Sham inafungamana na siasa za Magharibi hususan kutokuwa tishio kwa utawala wa Kizayuni wa Israel.
Utumiaji huu wa fimbo na bakora ya vikwazo vya Magharibi unafanywa dhidi ya nchi zote huru na zinazojitawala. Sera hii pia inatumika dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wananchi wa Syria pia ni wahanga wa vikwazo vya kikatili vya nchi za Magharibi.