UNICEF: Watoto 15,000 wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121614-unicef_watoto_15_000_wameuawa_gaza_tangu_oktoba_2023
Mfuko wa Kudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto wasiopungua 15,000 wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vyake dhidi ya ukanda huo Oktoba 7 mwaka 2023.
(last modified 2025-01-18T23:09:26+00:00 )
Jan 18, 2025 23:09 UTC
  • UNICEF: Watoto 15,000 wameuawa Gaza tangu Oktoba 2023

Mfuko wa Kudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) umetangaza kuwa, watoto wasiopungua 15,000 wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu utawala wa Kizayuni wa Israel ulipoanzisha vita vyake dhidi ya ukanda huo Oktoba 7 mwaka 2023.

Msemaji wa Mfuko wa Kuhudumia Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) amesema kuwa, watoto 35 wa Kipalestina hufariki dunia kila siku katika Ukanda wa Gaza kutokana na hujuma za utawala huo ghasibu dhidi ya taifa la Palestina.

James Elder amebainisha kwamba, kwa mujibu wa takwimu za vituo vya tiba, watoto 15,000 wa Kipalestina wameuawa katika Ukanda wa Gaza tangu Oktoba mwaka jana.

Wiki iliopita, Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Watoto (UNICEF) ulionya kuwa karibu watoto wote milioni 1.1 katika Ukanda wa Gaza wanakabiliwa na mgogoro wa afya ya akili na wanahitaji msaada wa kisaikolojia, huku utawala wa Israel ukiendeleza vita vya kikatili dhidi ya wakazi wa eneo hilo linalozingirwa.

Katika upande mwingine, Zaher Al-Wahidi, Mkurugenzi wa kitengo cha takwimu cha Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Gaza amesema, tangu kuanza vita vya Gaza Oktoba 7, 2023 hadi mwishoni mwa mwaka uliomalizika hivi karibuni (2024), kesi 4,500 za kukatwa kwa miguu sehemu ya juu au ya chini zimerekodiwa ikiwa ni matokeo ya mashambulizi ya anga na ardhini yanayoendelea kufanywa na utawala wa Kizayuni.