Wapalestina waanza kurejea makwao baada ya kuanza kutekelezwa usitishaji vita Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i121654-wapalestina_waanza_kurejea_makwao_baada_ya_kuanza_kutekelezwa_usitishaji_vita_gaza
Maelfu ya wakimbizi wa ndani wa Gaza walianza kurejea makwao asubuhi ya jana Jumapili baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya usitishaji vita baina ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala haramu wa Israel.
(last modified 2025-01-19T23:19:52+00:00 )
Jan 19, 2025 23:19 UTC
  • Wapalestina waanza kurejea makwao baada ya kuanza kutekelezwa usitishaji vita Gaza

Maelfu ya wakimbizi wa ndani wa Gaza walianza kurejea makwao asubuhi ya jana Jumapili baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya usitishaji vita baina ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na utawala haramu wa Israel.

Foleni ndefu ya watu waliobeba nguo na vitu vingine inaweza kuonekana kwenye picha zilizochapishwa na wapiga picha katika eneo hilo.

Vile vile kunaonekana msafara wa magari, mengine yalijaa watu walioshika bendera ya Palestina.

Huko Gaza kwenyewe Wapalestina walionekana wakisherehekea kuanza utekelezaji wa makubaliano ya usitishaji vita.

Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Palestina (UNRWA), ambalo linasema maelfu ya malori yenye chakula na unga sasa yanasubiri kuingia Gaza jambo lililokubaliwa katika mpango wa kusitisha mapigano.

Katika ujumbe kwenye mtandao wa X, shirika hilo linasema lina "malori 4,000 ya misaada tayari kuingia Gaza - nusu yao yanabeba chakula na unga".

Mkuu wa shirika hilo Philippe Lazzarini anaongeza: "Mashambulizi dhidi ya misafara ya misaada katika Ukanda wa Gaza yanaweza kupungua wakati misaada ya kibinadamu inakuja kufuatia kusitishwa kwa mapigano".

Katika upande mwingine, Chama cha siasa kali za mrengo wa kulia cha Jewish Power kimetangaza kuwa kinajitoa katika serikali ya Israel kwa kupinga makubaliano ya kusitisha mapigano, na kumuacha Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akiwa amesalia na wabunge wachache. Waziri wa usalama wa taifa Itamar Ben-Gvir, pamoja na Yitzhak Wasserlauf na Amichai Eliyahu, wamewasilisha barua zao za kujiuzulu leo ​​asubuhi.