UN: UNRWA inaendelea kufanya kazi licha ya vikwazo vya Israel
Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) litaendelea na shughuli zake licha ya vikwazo vilivyowekwa na utawala wa Israel.
Msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric, amesema katika mkutano na waandishi wa habari kwamba: "Tunawasiliana na wenzetu wa UNRWA katika kanda ya Asia Magharibi, na wanaendelea kutimiza wajibu wao na kutoa huduma."
Dujarric amesema kliniki za UNRWA huko Quds Mashariki (Jerusalem Mashariki) na Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu bado ziko wazi, na shughuli za misaada ya kibinadamu zinaendelea huko Gaza.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza: "UNRWA imedhamiria kubaki katika eneo hilo na kutekeleza majukumu yake, ndiyo maana bendera ya Umoja wa Mataifa bado inapepea juu ya majengo ya shirika hilo."
Siku ya Alhamisi, Januari 30, Israel ilianza kutekeleza uamuzi wa baraza la mawaziri la utawala huo wa kusitisha shughuli za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi wa Kipalestina (UNRWA) katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu na Jerusalem Mashariki.
Utawala haramu wa Israel umehalalisha hatua yake hiyo kwa kuibua madai yasiyo na msingi kwamba, baadhi ya wafanyakazi wa UNRWA walishiriki katika Operesheni ya Kimbunga cha al Aqsa dhidi ya vitongoji vya walowezi wa Kizayuni na kambi za kijeshi za utawala huo ghasibu tarehe 7 Oktoba 2023. Hadi sasa Israel imeshindwa kuthibitisha madai hayo.
Umoja wa Mataifa umesisitiza kwamba UNRWA itaendelea kuheshimu msingi wa kutoegemea upande wowote na dhamira yake ya kuendeleza shughuli zake za kibindamu na kupinga marufuku ya utawala ghasibu wa Israel.