Hali ya hatari Myanmar yarefushwa, Waislamu wa Rohingya wanaendelea kuteseka
Utawala wa kijeshi wa Myanmar umerefusha muda wa hali ya hatari kwa miezi sita zaidi, siku moja kabla ya kuadhimisha mwaka wa nne wa mapinduzi nchini humo.
Kwa sasa Myanmar imetumbikia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe katika mikoa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na katika maeneo ya karibu na mpaka wa China. Vilevile Waislamu wa Rohingya, ambao wanaendelea kukabiliwa na mashambulizi makali ya wanajeshi na Mabudha wenye itikadi kali, wako katika hali ya sintofahamu. Licha ya ombi la Umoja wa Mataifa, serikali ya kijeshi ya Myanmar haiko tayari kukubali kuwajibika na kutatua matatizo ya jamii hiyo ya Waislamu wala kujadili suala la kurejea wakimbizi wa Rohingya kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Bangladesh.
Hali hii imeifanya serikali ya Bangladesh kuwapeleka wakimbizi wa Rohingya ambao ni zaidi ya watu milioni moja, kwenye kambi za visiwa vya mbali ambavyo havina mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuishi binadamu.
Zaidi ya watu milioni tatu, wengi wao wakiwa Waislamu wa Rohingya waliofurushwa katika maeneo mbalimbali ya Myanmar, wamekimbia makazi yao kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe, na wamepewa hifadhi katika nchi za eneo hilo kama Bangladesh, Malaysia, India, Thailand na Indonesia.
Umoja wa Mataifa, umeituhumu serikali ya kijeshi ya Myanmar kuwa imehusika na mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu, na umetoa wito wa kutayarishwa mazingira yanayofaa kwa ajili ya kuwarejesha wakimbizi nchini Myanmar. Wakati huo huo Umoja wa Mataifa umetoa wito wa kukomeshwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Myanmar kupitia njia ya mazungumzo na kusaidia mchakato wa kutatua matatizo ya wananchi wa nchi hiyo.
Mwezi uliopita, jeshi la Myanmar lilikiangamiza kijiji cha Waislamu katika jimbo la Rakhine katika duru mpya ya jinai na uhalifu unaofanywa na Mabudha dhidi ya Waislamu.
Ripoti zinasema, takriban watu 41 wameuawa na wengine 52 kujeruhiwa katika shambulio la bomu kwenye kijiji cha Kyauk Ni Maw, kilichoko kusini mwa Kisiwa cha Ramree, ambacho wakazi wake wengi Waislamu wa makabila la Rohingya na Kayan katika Jimbo la Rakhine.
Ni zaidi ya muongo mmoja sasa ambapo Mabudha wenye misimamo mikali pamoja na jeshi la Myanmar wamekuwa wakifanya jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya hususan katika Jimbo la Rakhine. Lengo muhimu zaidi la uhalifu huo ni kuyageuza maeneo ya makazi na mashamba ya Warohingya kuwa ardhi iliyoungua na hatimaye kuinyakua.
Sababu inayotolewa kuhalalisha uhalifu huo wa kuwaua na kuwafukuza Waislamu wa Rohingya ni kwamba wao ni wahajiri walioingia Myanmar kutoka Bangladesh na lazima waondoke nchini humo. Hii ni licha ya kwamba, ushahidi wa kihistoria unaonyesha kuwa Waislamu wa Rohingya ni wenyeji asilia wa Myanmar hususan katika Jimbo la Rakhine, bali pia walitawala eneo hilo kwa mamia ya miaka.
Mabudha wenye misimamo mikali na wanajeshi wa Myanmar walikuwa wamesimamisha kwa muda mauaji ya Waislamu wa Rohingya kutokana na malalamiko ya kimataifa, lakini hivi sasa ambapo jamii ya kimataifa inashughulishwa na masuala kama vile hali ya Asia Magharibi na Ukraine, wameona ni vyema kuendeleza jinai zao huko Myanmar.
Alaa kulli hal, kinachowasumbua zaidi Waislamu wa Rohingya nchini Myanmar na kuwa sababu ya kuendelezwa ukandamizaji dhidi yao ni hatua ya serikali ya kukataa kuwapa haki za uraia.
Kwa sasa, theluthi moja ya wakazi wa Myanmar wanahitaji misaada ya kibinadamu, na wenzo pekee wa kuwashinikiza wanajeshi wanaotawala nchi hiyo ni Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN). Myanmar ni mwanachama katika jumuiya hiyo, lakini kwa kuzingatia kwamba, kwa mujibu wa sheria za ASEAN, taasisi hiyo haiwezi kuingilia masuala ya ndani ya wanachama wake, nchi pekee zenye ushawishi kwa serikali ya kijeshi ya Myanmar ni China na kwa kiasi fulani, India. Hivyo watu wa Myanmar hususan jamii ya Waislamu wa Rohingya, wanatarajia kuona nchi hizo zikichukua hatua za kuhakikisha wanapewa msaada wa kutatua matatizo ya nchi hiyo.