Netanyahu: Saudia imege ardhi yake na kuwapatia Wapalestina waunde nchi yao
Feb 08, 2025 02:30 UTC
Waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu amependekeza Wapalestina waunde nchi yao ndani ya Saudi Arabia badala ya kwenye ardhi ya nchi yao ya asili; na ametupilia mbali dhana yoyote ya kuwepo nchi ya Palestina yenye mamlaka kamili ya kujitawala.
"Wasaudi wanaweza kuunda nchi ya Palestina ndani ya Saudi Arabia; wana ardhi nyingi huko," alisema Netanyahu siku ya Alkhamisi katika mahojiano na Idhaa ya 14 ya Israel huku akipuuza matakwa ya muda mrefu ya Wapalestina ya kujitawala na kuwa na nchi yao huru.
Alipoulizwa kama kuundwa nchi ya Palestina ni muhimu kwa ajili ya kuanzisha uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Saudi Arabia, waziri mkuu huyo wa utawala wa Kizayuni alipinga wazo hilo akidai kuwa ni "tishio la usalama kwa Israel".
“Hasa nchi ya Palestina", amedai Netanyahu na kuongezea kwa kuhoji: baada ya Oktoba 7? Je! unajua hiyo ni nini? Kulikuwa na nchi ya Palestina, ikiitwa Ghaza. Ghaza, inayoongozwa na Hamas, ilikuwa nchi ya Palestina na angalia tulichopata".
Katika mahojiano hayo, Netanyahu alizungumza pia uwezekano wa kuanzishwa uhusiano rasmi kati ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel na Saudi Arabia na kutabiri kufikiwa karibu makubaliano hayo.
"Nadhani amani kati ya Israel na Saudi Arabia sio tu inawezekana, nadhani itafanyika", alisisitiza waziri mkuu huyo wa Israel.
Hata hivyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imetupilia mbali maelezo ya Netanyahu ya kusisitiza kwamba kuanzisha uhusiano rasmi na Israel si suala la kujadiliwa kabla ya kuundwa nchi ya Palestina, msimamo ambao Netanyahu anaendelea kuupuuza.../
Tags