Arab League yalaani wazo la Netanyahu la kuwahamishia Wapalestina Saudia
(last modified Mon, 10 Feb 2025 11:26:05 GMT )
Feb 10, 2025 11:26 UTC
  • Arab League yalaani wazo la Netanyahu la kuwahamishia Wapalestina Saudia

Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu amelaani vikali matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, ambaye alipendekeza kuwa Saudi Arabia inaweza kuunda taifa la Palestina ndani ya ardhi yake.

Ahmed Aboul Gheit amesema matamshi hayo ya Netanyahu "hayakubaliki na yanaonyesha namna alivyojitenga kabisa na uhalisia," akisisitiza kwamba mawazo kama hayo si kitu kingine isipokuwa njozi na ndoto za alinacha.

Aboul Gheit, kupitia kwa msemaji wake rasmi Gamal Roshdy, amekariri kwamba, Taifa la Palestina lazima liundwe katika ardhi iliyokaliwa kwa mabavu mwaka 1967, na Mashariki ya al-Quds kama mji mkuu wake, ikijumuisha Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Ukanda wa Gaza kama ardhi moja isiyoweza kugawanyika.

Matamshi hayo ya Katibu Mkuu wa Arab League yamekuja baada ya waziri mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel, Benjamin Netanyahu kusema kijuba kwamba, kama Saudia wanataka Wapalestina wawe na nchi yao, basi wawamegee eneo ndani ya ardhi ya Saudi Arabia ili waunde nchi yao, na sio kwenye ardhi ya nchi yao ya asili.

Netanyahu, Waziri wa Jinai

Kabla ya hapo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudi Arabia ilipongeza upinzani wa kimataifa dhidi ya matamshi hayo ya Netanyahu kuhusiana na Ukanda wa Gaza, na imepinga hatua yoyote ya kuhamishwa Wapalestina kutoka kwenye ardhi zao. 

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Saudia imesema: Watu wenye misimamo mikali na ya kibeberu hawaelewi maana ya ardhi ya Palestina wala mfungamano mkubwa na wa kidamu walio nao Wapalestina na adhi zao hizo.