Misri yatayarisha mpango mbadala wa kukabiliana na wa Trump huko Gaza
(last modified Sun, 02 Mar 2025 07:28:50 GMT )
Mar 02, 2025 07:28 UTC
  • Misri yatayarisha mpango mbadala wa kukabiliana na wa Trump huko Gaza

Vyanzo vya habari vya Misri vimeripoti kuwa Cairo imetupilia mbali mpango wa Rais wa Marekani, Donald Trump kuhusu eneo la Ukanda wa Gaza huko Palestina na sasa imetayari mpango mbadala.

Duru za Misri zimetangaza kuwa Cairo imekamilisha kuandaa mpango wake wa kujenga upya Ukanda wa Gaza bila ya kuwafukuza wakazi wake, tofauti na mpango uliopendekezwa na Donald Trump.

Duru hizo zimeongeza kuwa: Mpango huo unajumuisha hatua tatu, kuanzia hatua ya  rasilimali watu hadi ujenzi wa Ukanda wa Gaza kwa ushirikisha wakazi wa ukanda huo.

Mpango huo umepangwa kuwasilishwa katika mkutano wa dharura wa viongozi wa nchi za Kiarabu utakaofanyika Cairo mnamo Machi 4.

Kwa mujibu wa mpango huo, kutaanzishwa maeneo ndani ya Ukanda wa Gaza kwa ajili ya makazi ya muda ya Wapalestina ili makampuni ya Misri na Kiarabu yaanze kazi ya kujenga upya eneo hilo lililoharibiwa na Israel.

Kamati ya utawala pia itachukua jukumu la kusimamia masuala ya Gaza wakati wa awamu ya mpito kwa muda wa miezi sita. Mamlaka ya Palestina pia itakuwa na utawala kamili katika ukanda huo.

Tarehe 4 Februari, Donald Trump alitangaza, wakati wa mkutano na waandishi wa habari akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu huko Washington, kwamba nchi yake italitwaa eneo la Gaza baada ya kuwafukuza Wapalestina.