Hamas: Tumejenga upya uwezo wetu kwa vita vyovyote vya siku zijazo
Kiongozi mmoja wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palesina HAMAS amesema kuwa, ingawa uamuzi wa kuanzisha tena vita kwa sasa unaonekana uko mbali, lakini harakati hiyo tayari imejenga upya uwezo wake wa kijeshi ili kukabiliana na vita vyovyote vile vya siku za usoni.
Bassam Khalaf amesema hayo na kuongeza kuwa: "Kuanzisha tena vita katika hali ya hivi sasa ni jambo gumu zaidi kuliko hata huko nyuma na hii inaonesha kiwango cha utayari wa Hamas wa kukabiliana na matukio yoyote yanayoweza kutokea katika siku za usoni."
Akizungumzia mkutano wa kilele wa Waarabu mjini Cairo, Khalaf amesema: "Hatushughulishwi na taarifa zilizovujishwa na vyombo vya habari kutoka ndani ya mkutano huo. Hamas inasubiri msimamo rasmi wa mkutano wa kilele wa Waarabu kuhusu matukio ya hivi karibuni."
Kiongozi huyo mwandamizi wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palesitna HAMAS vile vile amesisitiza kwamba, harakati hiyo ilikuwa ikishughulikia suala la kuunda serikali ya umoja wa kitaifa katika Ukanda wa Ghaza hata kabla ya vita na imekuwa ikitoa mwito wa mara kwa mara wa kuundwa serikali ya namna hiyo kwenye ukanda huo. Bassam Khalaf ameongeza kuwa: Hamas ilitoa pendekezo hilo la kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa kabla ya kuanza vita, lakini upinzani dhidi yake ulipelekea kutoundwa serikali hiyo na badala yake kuundwa kamati ya kijamii.
Kiongozi huyo wa ngazi ya juu wa Hamas pia amesema: "Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu anapinga serikali yoyote inayoongozwa na HAMAS kwenye Ukanda wa Ghaza lakini pia anapinga eneo hilo kuendeshwa na Mamlaka ya Ndani ya Palestina. Hataki kabisa kuweko utawala wa aina yoyote wa Wapalestina kwenye ukanda huo."