Amnesty yataka kuchunguzwa jinai za kivita za Israel nchini Lebanon
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limetoa mwito wa kufanyika uchunguzi huru juu ya mashambulizi ya utawala wa Israel dhidi ya vituo vya matibabu, magari ya dharura na wafanyakazi wa afya nchini Lebanon, na kutaja hujuma hizo kama uhalifu wa kivita.
Amnesty International imesema kuwa, "mashambulizi dhidi ya vituo vya matibabu na wafanyikazi ni ukiukaji wa sheria za kimataifa," ikisisitiza kwamba "vikosi vya misaada na vifaa vya matibabu viko chini ya ulinzi wa kimataifa" chini ya viwango hivi vya kisheria.
Mashambulizi ya Israel dhidi ya Lebanon yamesababisha vifo na uharibifu mkubwa wa miundomsingi nchini humo, jambo ambalo ni mfano wa uhalifu wa kivita.
Kwa mujibu wa Amnesty International, kati ya Oktoba 3 na 9, wafanyakazi wa misaada ya kibinadamu wapatao 19 waliuawa na 11 kujeruhiwa katika mashambulizi manne tofauti kwenye vituo vya matibabu.
Kadhalika shirika hilo la kutetea haki za binadamu limetangaza kuwa, magari 256 ya dharura, ikiwa ni pamoja na ambulensi na magari ya zima moto, yalilengwa kwenye hujuma hizo za Wazayuni.

Wizara ya Afya ya Lebanon imeripoti kwamba, kumekuwa na mashambulizi 67 dhidi ya hospitali, ambapo 40 yalilenga moja kwa moja vituo hivyo vya matibabu, na kusababisha vifo vya 16. Kadhalika mashambulizi 238 dhidi ya wahudumu wa dharura yamesababisha vifo vya watu 206.
Makadirio ya awali yanaonyesha kuwa, gharama ya kujenga upya maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya Israel huko kusini na mashariki mwa Lebanon, pamoja na vitongoji vya kusini mwa Beirut inaweza kupindukia dola bilioni 10.