Umuhimu wa Siku ya Kimataifa ya Quds katika uga wa kikanda na kimataifa
(last modified Sat, 29 Mar 2025 08:14:02 GMT )
Mar 29, 2025 08:14 UTC
  • Umuhimu wa Siku ya Kimataifa ya Quds katika uga wa kikanda na kimataifa

Maandamano ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds yalifanyika jana Ijumaa tarehe 28 Machi nchini Iran na katika miji na vijiji vya nchi nyingine duniani kwa mahudhurio makubwa ya watetezi wa Palestina.

Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani imepewa jina la Siku ya Kimataifa ya Quds, kutokana na ubunifu uliofanywa na mwasisi wa Jamhuri ya kiislamu ya Iran, hayati Imam Ruhullah Khomeini (RA), baada tu ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu hapo mwaka 1979.

Waislamu na wananchi waliokuwa katika funga ya Ramadhani nchini Iran na maeneo mengine ya dunia walishiriki kwa wingi katika maandamano ya Siku ya Quds, na kwa mara nyingine tena wametangaza uungaji mkono wao kwa watu wanaodhulumiwa wa Palestina na kulaani jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Masoud Pezeshkian, ambaye pia alishiriki katika maandamano hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds alikosoa kimya cha watetezi wa haki za binadamu na wanasiasa mbele ya jinai zinazofanywa na utawala ghasibu wa Israel na kusema: "Dhati ya mienendo ya utawala wa Kizayuni na wale wanaouuunga mkono utawala huo ni kutenda jinai, unyama na kukiuka sheria za kibinadamu." Rais Pezeshkian ameongeza kuwa: "Lazima tuiulize dunia ambayo wanasiasa wake wanadai kutetea haki za binadamu kwamba, ni dhambi gani wamefanya wanawake na watoto wasio na hatia wanaomiminiwa mabomu na utawala wa Kizayuni na kuchomwa moto chini ya vifusi vya nyumba zao na kwa kutumia vibaya sayansi na teknolojia ya kisasa? Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "Mienendo  ya kijinai ya utawala wa Kizayuni ni jambo lisilotasawarika na lisilokubalika."

Rais Pezeshkian akiwa katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds, Tehran

Katika azimio la mwisho la maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds mjini Tehran, waandamanaji waliitaja Siku ya Kimataifa ya Quds kuwa ni kielelezo halisi cha kaulimbiu inayosema: "Siku ya Quds ni Siku ya Ushindi" na nukta ya kukutana pamoja katika mapambano ya dunia dhidi ya Uzayuni na kufichua mbinu za mfumo wa ubeberu wa kimataifa. Vilevile wameitaja Palestina kuwa kadhia ya kwanza ya Ulimwengu wa Kiislamu na kitovu cha mpambano wa kihistoria kati ya Muqawama wa Kiislamu na miradi ya kibeberu na kibepari ya kimataifa. 

Vilevile wamelaani jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel na kuzitaka jumuiya za kimataifa kuchukua hatua haraka iwezekanavyo ili kukomesha jinai hizo dhidi ya binadamu na kuwahukumu viongozi wa utawala wa Kizayuni. 

Uvamizi na kujitanua zaidi utawala ghasibu wa Israel kunakofanyika kupitia unyanyasaji wa kimfumo, vimesababisha ukiukwaji mkubwa na wa kimfumo wa haki za watu wa Palestina kwa miaka mingi. Mwenendo huu ambao unaungwa mkono na kusaidiwa na Marekani na serikali za nchi za Magharibi, unahesabiwa kuwa tishio kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa, na unafanyika kwa malengo ya muda mrefu ya kuzusha mifarakano na kuugawa Ulimwengu wa Kiislamu. Kwa msingi huo, Siku ya Kimataifa ya Quds ni harakati si tu ya kulaani uvamizi huo, bali pia ni ishara ya mwamko wa Umma wa Kiislamu dhidi ya njama ambazo Marekani, utawala wa Kizayuni wa Israel na waitifaki wao wanatekeleza katika eneo hili.

Aidha sera ya vikwazo ya serikali za nchi za Magharibi hususan Marekani imekuwa ikitumika kuuunga mkono utawala wa Kizayuni. Lengo la hatua zote hizo ni kuwakatisha tamaa wananchi wa Palestina ili wasitishe Muqawama na mapambano yao ya ukombozi dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na kuwalazimisha Wapalestina kufanya mapatano na utawala huo ambao umeshindwa kufikia lengo hilo la kimsingi na la kistratijia hadi leo.

Operesheni ya "Kimbunga cha Al-Aqsa" ilikuwa kielelezo kizuri katika uwanja wa Muqawama wa Palestina na kusimama kidete dhidi ya njama na malengo maovu ya Marekani na utawala wa Kizayuni katika eneo la Magharibi mwa Asia.

Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds mwaka huu wa 2025, yamefanyika katika hali ambayo maoni ya umma katika ulimwengu wa Kiislamu na duniani kote, yanashuhudia jinai za kutisha za Wazayuni huko Gaza, na vilevile mauaji ya kimbari yanayoendelea hadi leo katika eneo hilo. Kufanyika maadhimisho hayo ya Siku ya Kimataifa ya Quds kunaonyesha umoja wa Waislamu duniani kote katika kuitetea Palestina, mapambano yao ya ukombozi na haki zao halali. 

Quds Day, Kenya

Siku ya Kimataifa ya Quds daima imekuwa ishara ya mshikamano wa Ulimwengu wa Kiislamu katika kuiunga mkono Palestina, na alama ya kuongezeka mazingatio na mwamko wa makundi mbalimbali ya watu hususan vijana.

Vyombo vya habari vya Magharibi vimeshindwa katika malengo na mipango yao ya kupunguza umuhimu wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Quds. Mahudhurio makubwa ya watu katika miji ya nchi mbalimbali duniani ni dhihirisho la umuhimu wa siku hii na taathira zake katika mshikamano na mwamko wa watu duniani kote katika kuwaunga mkono na kuwatetea watu wa Palestina.