Wimbi jipya la utiaji nguvuni wapinzani lashuhudiwa nchini Bahrain
Vikosi vya utawala wa Aal Khalifa limemtia nguvuni Mkuu wa Baraza la harakati ya al-Wifaq na viongozi wengine kadhaa wa kidini wa nchi hiyo.
Katika kuendeleza ukandamizaji dhidi ya upinzani na kuzidisha mbinyo na mashinikizo kwa wananchi wa Bahrain, vikosi vya usalama vya utawala wa Manama vimemtia mbaroni Jamil Kadhim, Mkuu wa Baraza la harakati al-Wifaq pamoja na watu wengine saba wakiwemo mashekhe na wasomaji kasida za kuwasifu Ahlul Bayt wa Bwana Mtume SAW.
Katika upande mwengine vyombo vya usalama vya Bahrain vimewaweka kizuizini baba wa baadhi watu waliouliwa katika vuguvugu la Mapinduzi ya nchi hiyo.
Wakati huohuo Mkuu wa Mashtaka wa Bahrain ametangaza kuwa muda wa hukumu ya kuwekwa kizuizini sheikha Majid al Mash'al, mkuu wa baraza la Maulamaa wa Bahrain ni siku 15.
Vikosi vya usalama vya utawala wa Aal Khalifa, asubuhi ya tarehe 30 Julai viliivamia nyumba ya Sheikh Majid al-Mash'al na kumtia nguvuni alimu huyo wa Kishia bila ya kumweleza sababu wala tuhuma zinazomkabili.
Tangu mwezi Februari mwaka 2011, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya kupinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.
Wananchi wa Bahrain wanataka uhuru, kutekelezwa uadilifu, kuondolewa ubaguzi na kuweko madarakani utawala uliochaguliwa na wananchi wenyewe. Hata hivyo utawala wa Aal Khalifa umekuwa ukijibu matakwa ya wananchi hao kwa mkono wa chuma na ukandamizaji.../