Mhariri Mkuu wa Middle East Eye: Harakati ya HAMAS katu haitasalimu amri
Apr 25, 2025 07:23 UTC
David Hearst, Mhariri Mkuu wa tovuti ya habari ya Middle East Eye amesema, Muqawama ndio njia pekee iliyobaki kwa ajili ya kukomesha ughasibu na kukaliwa kwa mabavu ardhi za Palestina na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Hearst, ambaye pia ni mchambuzi na mwasisi wa tovuti ya Middle East Eye ameeleza katika makala aliyoandika kwamba utawala wa Kizayuni unapaswa uelewe kuwa Hamas kamwe haitasalimu amri na akafafanua kwa kusema: "leo kusalimu amri Hamas na Ghaza kutamaanisha kusalimu amri kadhia nzima ya Palestina, ilhali Muqawama ndio njia pekee iliyobaki ya kukomesha ukaliaji ardhi kwa mabavu".
Mwandishi huyo Muingereza ameendelea kueleza katika makala yake hiyo kwa kusema: madai kwamba viongozi wa Hamas huko Ghaza wamepokea kiasi kikubwa cha fedha na kutoroka- wakati miezi 18 imepita ya vita vya pande zote na miezi miwili ya watu kuteswa kwa njaa katika Ukanda wa Ghaza-, yanadhihirisha uelewa na ufahamu finyu alionao waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu Hamas.
Hearst ameongeza kuwa: Hamas haijarudi nyuma katika masharti yake mawili ambayo iliyasisitiza mwanzoni mwa vita, nayo ni kutoweka chini silaha, kuondoka kikamilifu majeshi ya Israel katika Ukanda wa Ghaza, na kukomeshwa vita hivyo.
Mhariri huyo wa tovuti ya Middle East Eye amesema: "suala hili limekuwa likisisitizwa mara kwa mara na kwa uwazi kwamba Netanyahu ndiye kikwazo kikuu cha kupatikana suluhu kwa njia ya mazungumzo kwa sababu alisaini mara mbili hati za makubaliano na Hamas na baada ya kufanya hivyo akachukua hatua ya upande mmoja ya kuyakiuka makubaliano hayo".../
Tags