Afisa wa Hospitali ya Nasser: Maisha ya maelfu ya watoto katika Ukanda wa Gaza yako hatarini
(last modified Fri, 02 May 2025 07:25:42 GMT )
May 02, 2025 07:25 UTC
  • Afisa wa Hospitali ya Nasser: Maisha ya maelfu ya watoto katika Ukanda wa Gaza yako hatarini

Mkuu wa kitengo cha watoto katika Hospitali ya Nasser iliyoko kusini mwa Gaza ametahadharisha kuhusu kukithiri kwa utapiamlo miongoni mwa watoto katika ukanda huo na hatari inayotishia maisha ya maelfu ya watoto kutokana na siasa za ufashisti za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Dk Ahmed Al-Fara amesisitiza kuwa: "Hali ya afya imefikia hatua mbaya ambayo inatishia maisha ya maelfu ya watoto kutokana na kuporomoka kusiko na kifani kwa mifumo ya chakula na afya."
Al-Fara amesema: "Ukanda wa Gaza unakabiliwa na mgogoro hatari wa kiafya, na kesi mbaya za utapiamlo miongoni mwa watoto zimeongezeka katika wiki za hivi karibuni."

Mkuu wa kitengo cha watoto katika Hospitali ya Nasser ameongeza kuwa: "Taarifa za afya zinaonyesha kuwa zaidi ya watoto 52 wamekufa kutokana na njaa na utapiamlo tangu kuanza kwa vita, huku ripoti za Umoja wa Mataifa zikionyesha kuwa watu milioni 2.4 wa Gaza wako katika hatari ya njaa, na hii inatokana na kuzorota kwa kasi kwa masuala ya kibinadamu."

Dk. Al-Fara amesisitiza kuwa: "Watoto wachanga ndio wanaoathirika zaidi kwa sababu kwa ujumla hutegemea maziwa ya mama zao, na kutokana na utapiamlo wa mama, maisha ya mtoto yako hatarini hasa kwa vile maziwa ya unga pia ni haba na bei yake sokoni inapanda sana."

Mkuu wa kitengo cha watoto katika Hospitali ya Nasser kusini mwa Gaza ametoa wito wa kuingilia kati mara moja Umoja wa Mataifa na mashirika ya afya na misaada ya kibinadamu ili kuokoa maisha ya watoto wa Gaza akisema: "Hali mbaya katika Ukanda wa Gaza inahitaji hatua za haraka kuokoa maisha kabla ya wakati kutoweka."