Kushadidi njama za utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Quds
Ripoti mbalimbali zinaonesha juu ya kuanza duru mpya ya njama za utawala wa Kizayuni wa Israel za kutaka kuwa na satua katika mji wa Quds.
Jambo hilo linabainisha wazi wigo mpana na hatari zaidi wa njama za Wazayuni katika mji wa Quds baada ya kuundwa Baraza la Mawaziri lenye misimamo mikali la Benjamin Netanyahu Waziri Mkuu wa utawala bandia wa Israel. Kwa hakika hatua hizo zimeibua wimbi la wasiwasi mkubwa miongoni mwa Wapalestina na fikra za waliowengi ulimwenguni.
Katika uwanja huo, Waziri wa Masuala ya Quds katika serikali ya Palestina ametoa indhari kuhusiana na hatua za uharibifu za utawala huo ghasibu huko Quds.
Siku ya Jumatano Adnan Husseini, Waziri wa Masuala ya Quds katika serikali ya Palestina sambamba na kutahadharisha kuhusiana na njama za Israel huko Quds alisema kuwa, hatua hizo ni sehemu ya mipango ya wazi ya kuwafukuza Wapalestina kutoka katika miji yao, kupanua satua ya Wazayuni katika maeneo na milki za Wapalestina huko Quds, kubadilisha utambulisho wa Msikiti wa al-Aqswa na kuongeza uingiliaji katika masuala ya uongozi na usimamizi wa Waqfu za Kiislamu.
Hii ni katika hali ambayo, siku chache zilizopita pia, Wizara ya Wakfu na Masuala ya Kidini ya Palestina ilitangaza kuwa, wanajeshi na walowezi wa Kizayuni mwezi uliopita walivamia na kuyavunjia heshima matukufu ya Kiislamu mara 87 na kuongeza kuwa, katika kipindi chote cha mwezi uliopita kila siku Wazayuni walivamia na kufanya hujuma dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa.
Hatua zenye kiburi za utawala wa Kizayuni wa Israel haziishii tu katika kufanya uharibifu na kujitanua huko Baytul Muqaddas bali maeneo mengine pia daima yamekuwa yakiandamwa na Wazayuni hao na hatua hizo zinaonekana kushika kasi mno katika miezi ya hivi karibuni.
Hujuma na uvamizi wa mara kwa mara wa Wazayuni dhidi ya Masjid al-Aqswa na uchochezi wao wa kubomoa maeneo hayo matakatifu ni mambo yanayofanyika kwa lengo la kufuta utambulisho wa Kiislamu wa mji huo. Takwimu na ripoti mbalimbali zinaonesha kuwa, mwenendo huu wa kuyaandama kwa hujuma maeneo hayo hususan huko Baytul Muqaddas umeongezeka mno katika mwaka huu wa 2016. Mwanzoni mwa mwaka huu walimwengu wameshuhudia kushadidi hujuma za utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Msikiti wa al-Aqswa kibla cha kwanza cha Waislamu na takribani kila siku msikiti huo umekuwa ukikabiliwa na njama za kuuvunjia heshima zinazofanywa na Wazayuni.
Tangu utawala ghasibu wa Israel utangaze uwepo wake, umebomoa mamia ya misikiti na kuisababishia hasara mamia ya misikiti mingine. Utawala huo vamizi umekuwa ukifanya kila uwezalo kuyapa sura ya Kizayuni maeneo ya Wapalestina na katika kusukuma mbele gurudumu lake hilo, umelipa kipaumbele suala la kubomoa athari za Kiislamu, nyumba na majengo ya kihistoria ya Wapalestina.
Kutokana na kushadidi hatua hizo, tangu mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka uliopita hadi sasa maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu yamekuwa yakishuhudia wimbi la malalamiko ya upinzani dhidi ya siasa za kichokozi za utawala wa Kizayuni na njama za utawala huo za kuvuruga utambulisho wa Baitul Muqaddas pamoja na mpango wake wa kuugawa kiwakati na kimahali msikiti mtukufu wa Al-Aqsa. Wimbi hilo la malalamiko limekuwa maarufu kwa jina la Intifadha mpya ya Quds.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, radiamali hizo za Wapalestina mkabala na hatua za kupenda kujitanua za Israel huko Baytul Muqaddas na hatua za kichochezi za Wazayuni zinaonesha unyeti walionao Wapalestina kuhusiana na kadhia ya Quds na ndio maana wamesimama kidete na kufanya hima kulilinda eneo hilo takatifu kwa nguvu zao zote.