Mizizi ya ukoloni katika mzozo wa India na Pakistan
Mzozo wa India na Pakistan ni moja ya migogoro sugu na ya muda mrefu zaidi katika eneo la Asia Kusini.
Mizizi ya mzozo huo inarudi nyuma hadi enzi za ukoloni wa Uingereza, na nafasi yake katika kuchochea mgogoro huo haiwezi kufumbiwa macho. Ikiwa mkoloni India, Uingereza ilichukua maamuzi na hatua za kihistoria, kiuchumi na kisiasa, ambazo huchochea mara kwa mara migogoro kati ya India na Pakistan, migogoro ambayo imekuwepo kati ya nchi hizo tangu kugawanywa kwa bara Hindi mnamo 1947.
Baada ya uamuzi wa Uingereza wa kuondoka India mwaka 1947, ambao ulikuja baada ya mapambano ya muda mrefu dhidi ya ukoloni yaliyoongozwa na Mahatma Gandhi na Muhammad Ali Jinnah, mchakato wa kuunda nchi mbili huru za India na Pakistan ulifanyika, suala ambalo baadaye lilichochea mgogoro kati ya nchi hizo mbili, hasa kuhusu kadhia ya Kashmir. India iligawanywa katika misingi ya kikoloni katika nchi mbili huru: India (yenye Wahindu wengi) na Pakistani (yenye Waislamu wengi). Uchoraji wa mipaka na Mstari wa Radcliffe, bila kuzingatia hali halisi ya kijiografia na kiutamaduni, ulisababisha vurugu kubwa na kupelekea kuhamishwa mamilioni ya watu.
Mnamo 1945, serikali ya Uingereza, ikiongozwa na Waziri Mkuu wa wakati huo Clement Attlee, iliamua kukomesha utawala wa kikoloni wa India. Ili kusimamia mchakato huu, Lord Louis Mountbatten aliteuliwa kuwa Makamu wa mwisho wa Ufalme wa Uingereza nchini India mnamo Februari 1947. Mountbatten, ambaye aliwahi kuwa kamanda wa kijeshi katika Vita vya Pili vya Dunia, alipewa jukumu la kuandaa mazingira ya India kupewa uhuru kufikia Juni 1948, lakini ikafahamika kwamba tofauti kati ya Bunge la Kitaifa la India na Jumuiya ya Waislamu hazingeweza kutatuliwa na kwamba kugawanywa kwa bara hilo ndio suluhisho pekee lililowezekana.
Mountbatten alipendekeza mpango ambao ulijulikana kama "Mpango wa Mountbatten", ambao ulipelekea bara hilo dogo kugawanywa katika nchi mbili huru; India yenye Wahindu wengi na Pakistan yenye Waislamu wengi. Pakistani ilikuwa na sehemu mbili; Pakistan Magharibi (Pakistan ya sasa) na Pakistan ya Mashariki (Bangladesh ya sasa). Mpango huo uliidhinishwa mnamo Juni 1947, na tarehe ya uhuru ikaainishwa kuwa Agosti 15, 1947. Uingereza ilimchagua Sir Cyril Radcliffe, mwanasheria wa Uingereza asiye na uzoefu katika bara hilo, kuweka mipaka kati ya nchi hizo. Radcliffe alichora mistari ya mipaka ambayo baadaye ilijulikana kama "Radcliffe Line."

Mistari hii ilichorwa kulingana na wingi wa kidini na iliibua matatizo mengi. Kwa mfano katika jimbo la Punjab, mji kama Lahore, ambao ulikuwa na idadi ya Wahindu, Masingasinga na Waislamu, ulipewa Pakistan, na hivyo kusababisha uhamiaji na vurugu. Kashmir, eneo lenye Waislamu wengi linalotawaliwa na Hindu Maharaja, likawa suala kuu la mzozo. Baada ya Kashmir kutwaliwa na India mnamo 1947, Vita vya Kwanza vya India na Pakistani (1947-1948) vilianza, na hadi leo, Kashmir bado ni eneo linalozozaniwa. Radcliffe hakurejea tena katika bara hilo na baadaye alisema alijutia matokeo ya matendo yake. Maamuzi yake yalisababisha kuhama kwa takriban watu milioni 12 na vifo vya watu milioni 1 hadi 2 katika ghasia za kidini, uhamiaji mkubwa zaidi wa kulazimishwa katika historia.
Kugawanywa bara Hindi kati ya nchi mbili huru, India na Pakistan, kunaweza kuchukuliwa kuwa moja ya matukio muhimu zaidi katika karne ya 20, ambayo yalikuwa na matokeo makubwa katika bara la Asia na pia kimataifa. Kujiondoa kwa Waingereza kutoka India mnamo 1947 bila kufafanua muundo mpya wa kitaifa kulisababisha maafa na majeraha makubwa ya kihistoria ambayo bado yanasababisha mivutano na mapigano kati ya India na Pakistan.
India na Pakistan zilipotangaza uhuru wao, nchi hizi mbili changa zilikabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi, kisiasa na kijamii ambayo yalifanya ushirikiano kati yao na kutatua tofauti kuwa mgumu zaidi. Hali ya Kashmir, ambayo imekuwa jeraha la wazi kutokana na maamuzi mabaya ya Uingereza, bado ni sababu kuu ya mvutano na vita vingi kati ya India na Pakistan.
Mojawapo ya hatua hasi zaidi za Uingereza wakati wa Vita Baridi ilikuwa kuingizwa Pakistan katika mfumo wa usalama wa Magharibi kupitia uanachama wake katika Mkataba wa CENTO na msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo, hatua ambayo ilichochea mbio za silaha kati ya India na Pakistan. Mapema miaka ya 1950, Uingereza, pamoja na Marekani, ziliichagua Pakistan kama mshirika mkuu katika Asia ya Kusini, sehemu ya mkakati wa kudhibiti ukomunisti. Hatua hiyo ya upande mmoja kwa Pakistan iliisukuma India kwenye Umoja wa Kisovieti.
Uingereza pia ilibuni uchumi wa bara Hindi kutumika kama chanzo cha kudhamini malighafi na soko la watumiaji kwa viwanda vyake, suala ambalo halikutoweka hata baada ya kupatikana uhuru wa India na Pakistan mnamo 1947. Utegemezi huu wa kiuchumi na udhaifu wa kimuundo ulichochea ushindani wa kiuchumi, mizozo juu ya rasilimali za maji, na hivyo kuongeza mvutano kati ya nchi hizo mbili.