Kombora jingine la Yemen lapiga Tel Aviv mapema leo Alkhamisi
(last modified Thu, 22 May 2025 06:07:38 GMT )
May 22, 2025 06:07 UTC
  • Kombora jingine la Yemen lapiga Tel Aviv mapema leo Alkhamisi

Vyombo vya habari vya utawala wa Kizayuni wa Israel vimeripoti mapema leo Alkhamisi kwamba sauti za ving'ora vya tahadhari zimehinikiza katika maeneo mbalimbali ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni, kufuatia kombora lililorushwa kutoka Yemen ili kupiga maeneo muhimu mno ya Israel.

Duru mbalimbali zimenukuu taarifa za vyombo vya habari vya ndani ya utawala wa Kizayuni vikiripoti leo Alkhamisi kwamba ving'ora vya tahadhari vilikuwa vimewashwa katika sehemu kubwa ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na Wazayuni zilizopachikwa jina bandia la Israel. Havikuwashwa Tel Aviv pekee.

Kwa mujibu wa ripoti hizo, ving'ora hivyo vimesikika katika maeneo ya Tel Aviv, Rishon Letzion, Jaffa na Netanya baada ya kupokea ripoti za kurushwa kombora roketi kutoka Yemen.

Kwa upande wake, mtandao wa "Russia Today" umelinukuu jeshi la utawala wa Kizayuni likithibitisha habari ya kurushwa kombora kutoka Yemen na kudai kuwa mifumo ya ulinzi ya utawala wa Kizayuni ilikuwa inajaribu kulizuia.

Vyombo vya habari vinavyofuatilia taarifa za usafiri wa anga pia vimeripoti kuwa safari za ndege katika uwanja wa ndege wa Ben Gurion mjini Tel Aviv zimesitishwa kutokana na kombora lililorushwa kutoka Yemen.

Nao watumiaji wa mitandao ya kijamii wamerusha picha na video zinazoonesha kombora likipita kwenye anga ya ardhi za Palestina zinazokaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni.

Kanali ya 12 ya televisheni ya Israel imetangaza kuwa mfumo wa ulinzi wa anga wa utawala wa Kizayuni ulikuwa umewashwa kujaribu kukabiliana na kombora hilo la jeshi la Yemen.

Serikali ya Yemen imetangaza wazi kwamba itaendelea kuvifunga viwanja vya ndege na bandari za Israel kwa mashambulizi yake, hadi pale utawala wa Kizayuni utakapokomesha jinai zake huko Ghaza.