Hamas yaonya: Israel haitafikia malengo yake Ukanda wa Gaza
Utawala wa Israel umeanza kupeleka vikosi vya jeshi lake kwenye viunga vya Jiji la Gaza kwa ajili ya kuanza kutekeleza mpango wake wa kukalia kwa mabavu eneo hilo kubwa zaidi la Ukanda wa Gaza, lakini Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imeonya kuwa, Tel Aviv itashindwa kutimiza malengo yake.
Utawala wa Israel umeanzisha “Kitengo cha Kuhamisha Watu” ili kuanza kutekeleza kivitendo mpango wa kuwafukuza Wapalestina kutoka Jiji la Gaza kupitia kampeni ya mabango, ujumbe mfupi wa simu, na mizinga, hayo ni kwa mujibu wa vyombo vya habari vya utawala huo ghasibu.
Mpango huu unataka brigedi za kawaida kulizunguka jiji hili, ikilazimisha takriban wakazi milioni moja kuondoka. Operesheni hii kali ya uhamisho inasimamiwa na Kitengo cha Kuhamisha Watu cha Kamandi ya Kusini, ambacho uwepo wake umefichuliwa kwa mara ya kwanza hivi karibuni.
Jana Jumatano, jeshi la Israel liliripoti uzinduzi wa kile kinachoitwa "Operesheni ya Gideon Chariots II," mwendelezo wa mashambulio ya kikatili ya mwezi Mei, ambayo yalishuhudia utawala huo ukishadidisha pakubwa vita vyake vya mauaji ya halaiki vilivyoanza Oktoba 2023 katika Ukanda wa Gaza.
Waziri mkuu wa utawala huo pandikizi, Benjamin Netanyahu, mhandisi mkuu wa vita hivyo, ambaye anakabiliwa na hati ya kimataifa ya kukamatwa kwa mauaji ya halaiki, anatarajiwa kutoa "kibali cha mwisho" cha utekelezaji wa operesheni hiyo leo Alkhamisi. Hata hivyo, Hamas inasisitiza kuwa: "Utawala wa Kizayuni hautafikia malengo yake; na kwamba kuikalia kwa mabavu Gaza hayatakuwa matembezi kwenye bustani."
Utawala wa Kizayuni unaendeleza jinai na njama dhidi ya Gaza katika hali ambayo, HAMAS imesema kuwa imepasisha pendekezo jipya la Qatar na Misri la kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari vya Israel katika Ukanda wa Gaza.
Katika muda wa zaidi ya miaka miwili, Hamas imeafiki mapendekezo kadhaa kwa ajili ya kusitisha mapigano na kuwaachia huru mateka wa Israel na wafungwa wa Kipalestina. Hata hivyo Israel iliyakataa mapendekezo hayo na kuendelea mbele na kampeni yake ya kijeshi huko Gaza; ambapo sasa utawala huo unajitanua kuelekea katika Jiji la Gaza.