Hamas: US ni mshiriki wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i130134-hamas_us_ni_mshiriki_wa_jinai_za_israel_katika_ukanda_wa_gaza
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema hatua ya Marekani ya kutumia turufu dhidi maazimio ya Umoja wa Mataifa "inaifanya kuwa mshiriki" wa jinai za utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.
(last modified 2025-08-28T22:54:38+00:00 )
Aug 28, 2025 22:54 UTC
  • Hamas: US ni mshiriki wa jinai za Israel katika Ukanda wa Gaza

Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema hatua ya Marekani ya kutumia turufu dhidi maazimio ya Umoja wa Mataifa "inaifanya kuwa mshiriki" wa jinai za utawala wa Israel katika Ukanda wa Gaza.

Hamas imesema katika taarifa yake kwamba, inakaribisha taarifa ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ukiondoa Marekani, ambayo ilitaka "kusitishwa kwa mapigano mara moja, kupitia makubaliano ya kudumu na yasiyo na masharti" huko Gaza, ili kuruhusu msaada usio na kikomo katika eneo hilo la Palestina na kukomesha njaa.

Harakati hiyo ya Muqawama wa Kiislamu imeeleza baya kuwa, utawala haramu wa Israel unatumia njaa kama silaha, kitendo ambacho ni haramu na marufuku katika sheria ya kimataifa.

Nchi wanachama 14 kati ya 15 za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa - nne za kudumu, ambazo ni Russia, China, Uingereza na Ufaransa, na zingine 10 za zamu, zilitoa wito kwa utawala wa Israel siku ya Jumatano kuhitimisha vita vyake vya mauaji ya halaiki dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, ambavyo vimeacha mamia kwa maelfu ya majeruhi tangu kuanza kwake Oktoba 2023.

Marekani, mmoja wa wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la UN, haikushiriki katika kura hiyo, hatua ambayo ililipigisha chini azimio hilo la Umoja wa Mataifa.

Mauaji ya kikatili ya utawala ghasibu wa Israel dhidi ya Gaza tangu Oktoba 2023 yamesababisha vifo vya takriban Wapalestina 62,900 wengi wao wakiwa wanawake na watoto.

Hii ni katika hali ambayo, jamii ya kimataifa imeendelea kulaani jinai za Wazayuni katika Ukanda wa Gaza. Hivi karibuni, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine tena alisisitiza ulazima wa kusitishwa mara moja mapigano huko Gaza.