Walebanon waandamana Beirut wakipinga kupokoywa silaha Hizbullah
Wafuasi wa Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Lebanon za Hizbullah na makundi mengine ya Muqawama ya nchi hiyo wamefanya maandamano makubwa usiku wa kuamkia leo katika mji mkuu Beirut, wakipinga vikali pendekezo la baraza la mawaziri linaloungwa mkono na Marekani na Israel la kuwapokonya silaha wanamuqawama.
Shirika la habari la Iran Press limeandika habari hiyo na kueleza kuwa, waandamanaji hao wamelaani uingiliaji kati wa Marekani na Israel, na kutaja mpango huo wa upokonyaji silaha kama usaliti kwa uhuru wa kujitawala na haki ya kujilinda Lebanon.
Maandamano hayo yalijumuisha mikusanyiko ya hadhara ya waendeshaji pikipiki, misafara ya magari, na umati mkubwa wa watu waliokusanyika mitaani, hasa katika vitongoji vya kusini mwa Beirut (Dahieh).
Kwa mashinikizo ya mjumbe maalumu wa Marekani Tom Barak, Baraza la Mawaziri la Lebanon, liliamua katika kikao chake cha Agosti 5 kuidhinisha mpango wa kuipokonya silaha Hizbullah huku likipuuza sharti la kupatikana mwafaka wa jamii za nchi hiyo, kutokana na kikao hicho kufanyika bila kuhudhuriwa na mawaziri kutoka jamii ya Mashia.
Hatua hiyo ya baraza la mawaziri la Lebanon ilikabiliwa na mjibizo kutoka vyama vya Waislamu wa Kishia wa nchi hiyo. Katibu Mkuu wa Hizbullah, Sheikh Naim Qassem, aliikosoa vikali serikali ya Lebanon na kupinga maamuzi iliyopitisha hivi karibuni. Alibainisha kuwa, wajibu wa serikali ni kujenga nchi, na wala si kuikabidhi kwa adui.
Kadhalika Mawaziri wa Harakati za Muqawama wa Kiislamu za Lebanon za Hizbullah na Amal walitoka nje ya kikao cha Baraza la Mawaziri la nchi hiyo kupinga uwepo wa kamanda wa jeshi katika kikao cha serikali cha kujadili upokonyaji silaha za Muqawama.