Israel yampuuza Trump, yaendelea kuwaua Wapalestina Gaza; Hamas yalaani
Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina Hamas imemjia juu Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kwa madai ya uwongo kuwa ameliamuru jeshi la utawala huo kupunguza mashambulizi yake katika Ukanda wa Gaza.
Harakati hiyo imesema hayo katika taarifa yake ya jana Jumamosi baada ya Waziri Mkuu wa Israel kunukuliwa katika ripoti mbalimbali akidaiwa kuviagiza vikosi vya utawala huo "kusimamisha" mashambulizi yote katika eneo lote la Gaza, na eti kufanya tu mashambulizi ya "kujihami".
"Kuendelea kwa mashambulizi ya mabomu na mauaji ya uvamizi kunafichua uongo wa Netanyahu kuhusu kupunguza operesheni za kijeshi dhidi ya raia," Hamas imesema.
"Jeshi la utawala la Kizayuni linaendelea kufanya jinai na mauaji ya kutisha dhidi ya watu wetu wa Palestina katika Ukanda wa Gaza," imeeleza Hamas, ikisisitiza kwamba mashambulizi ya Israel ya punde zaidi yameua watu wasiopungua 70.
Kuendelea "kuongezeka kwa umwagaji damu kunaonyesha uwongo wa madai" yaliyotolewa na utawala huo "kuhusu kupunguzwa kwa operesheni za kijeshi dhidi ya raia wasio na silaha," kundi hilo limesema.
Hapo awali, Netanyahu aliripotiwa kutoa agizo hilo alipokuwa akilipa jeshi jukumu la "kuendeleza utayari" wa utekelezaji wa "sehemu ya kwanza" ya mpango wa vipengele 20 uliobuniwa na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Rais wa Marekani amedai kuwa pendekezo hilo linalenga kumaliza vita vya sasa vya mauaji ya halaiki vya tangu Octoba 2023 huko Gaza.
Hamas ilieleza kuridhia kwake na baadhi ya vipengele vya pendekezo hilo siku ya Ijumaa, ikisema itaingia kwenye mazungumzo ya kuwezesha kuachiliwa kwa mateka wa Israel waliosalia huko Gaza, walio hai na maiti.