Watu 40 wahukumiwa kifo Iraq kwa kuhusika na mauaji ya Speicher
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i1492-watu_40_wahukumiwa_kifo_iraq_kwa_kuhusika_na_mauaji_ya_speicher
Mahakama Kuu ya Jinai nchini Iraq imetoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa watu 40 baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji yaliyofanywa kwenye kambi ya kijeshi ya Speicher katika mji wa Tikrit, kaskazini mwa nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 18, 2016 13:06 UTC
  • Watu 40 wahukumiwa kifo Iraq kwa kuhusika na mauaji ya Speicher

Mahakama Kuu ya Jinai nchini Iraq imetoa hukumu ya adhabu ya kifo kwa watu 40 baada ya kupatikana na hatia ya kuhusika na mauaji yaliyofanywa kwenye kambi ya kijeshi ya Speicher katika mji wa Tikrit, kaskazini mwa nchi hiyo.

Watu hao 40 wamepatikana na hatia ya mauaji ya halaiki ya mwezi Juni mwaka 2014 ya mamia ya makuruta wa jeshi waliokuwa mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh huko kaskazini mwa Iraq.

Abdel Sattar Bayraqdar, msemaji wa vyombo vya mahakama vya Iraq amesema watu 40 waliopatikana na hatia wamehukumiwa adhabu ya kifo na wengine saba wameachiliwa huru kutokana na kukosekana ushahidi wa kutosha. Hata hvyo Bayraqdar hakufafanua jinsi watu hao walivyoshiriki katika mauaji hayo ya Speicher na namna walivyotiwa nguvuni.

Watu wengine 24 walihukumiwa adhabu ya kifo na kunyongwa mwezi Julai mwaka jana kwa kuhusika na mauaji hayo. Kwa mujibu wa maafisa wa Iraq magaidi wa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh waliua watu wapatao 1,700 katika kambi hiyo ya kijeshi ya Speicher mjini Tikrit.

Mnamo mwezi Juni mwaka 2014 magaidi wa Daesh walishambulia kambi hiyo iliyoko karibu na mji wa Tikrit na kuwashikilia mateka mamia ya askari vijana waliokuwepo kambini hapo.

Baadaye magaidi hao walisambaza mikanda ya video iliyoonyesha mateka hao wakiuliwa katika maeneo tofauti.

Wakati vikosi vya jeshi la Iraq vilipoukomboa mji wa Tikrit mwezi Machi mwaka jana viligundua mabaki ya viwiliwili 600 vya askari hao ambao wengi wao walikuwa wamezikwa kwenye makaburi ya umati.../