Duff: Kuchaguliwa Aoun kunaonesha Saudia inazidi kupoteza ushawishi
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i18610-duff_kuchaguliwa_aoun_kunaonesha_saudia_inazidi_kupoteza_ushawishi
Gordon Duff, Mhariri Mwandamizi wa jarida la Veterans Today la Marekani na pia mchambuzi wa masuala ya siasa amesema hatua ya Lebanon kupata rais mpya ni dhihirisho kuwa Saudi Arabia inazidi kupoteza ushawishi wake katika eneo la Mashariki ya Kati.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 01, 2016 15:08 UTC
  • Duff: Kuchaguliwa Aoun kunaonesha Saudia inazidi kupoteza ushawishi

Gordon Duff, Mhariri Mwandamizi wa jarida la Veterans Today la Marekani na pia mchambuzi wa masuala ya siasa amesema hatua ya Lebanon kupata rais mpya ni dhihirisho kuwa Saudi Arabia inazidi kupoteza ushawishi wake katika eneo la Mashariki ya Kati.

Katika mahojiano na kanali ya televisheni ya Press TV, Duff ambaye ni mkazi wa jimbo la Ohio nchini Marekani amesema nguvu na ushawishi wa Saudia katika eneo la Mashariki ya Kati unaelekea ukingoni, suala linaloonesha kuwa mahesabu yake ya kisiasa yamekuwa yakigonga mwamba kila uchao. Mchambuzi huyo wa masuala ya siasa wa Marekani amesema utawala wa Riyadh umekuwa 'ukimwaga pesa huku na kule' kuathiri mkondo wa siasa za Lebanon lakini umeshindwa kufua dafu. 

Michel Aoun, Rais mpya wa Lebanon

Amesema ubalozi wa Saudia mjini Beirut umekuwa ukitumika kama 'kituo cha kiintelijensia cha Riyadh' na kusisitiza kuwa, utawala huo wa kifalme unaunga mkono ugaidi bila kuficha.

Mhariri Mwandamizi wa jarida la Veterans Today ameongeza kuwa, licha ya makelele na madai ya Umoja wa Mataifa, lakini harakati ya Hizbullah ya Lebanon ndiyo jeshi pekee linalokabiliana na ugaidi nchini humo.

Michel Aoun amekula kiapo cha urais mbele ya wabunge wa nchi hiyo akiwa rais wa 13 wa Lebanon baada ya kiti hicho kusalia kitupu kwa karibu miaka miwili na nusu, tangu umalizike muda wa kuhudumu Michel Suleiman mwaka 2014.