Hashdu Shaabi: Hatuhitajii Marekani katika operesheni ya Mosul
Kikosi cha kujitolewa cha Hashdu Shaabi kinachoshirikiana na jeshi la Iraq katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul toka mikononi mwa kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh kimesema vikosi hivyo havihitajii muungano wa kijeshi wa Marekani katika mapambano hayo.
Sayyid Hamed Jazayeri, kamanda mkuu wa Hashdu Shaabi amesema kikosi hicho kina uzoefu na uwezo mkubwa wa kufanikisha operesheni hiyo pasina utegemezi wa muungano wa kijeshi wa Wamagharibi unaoongozwa na Marekani. Ameongeza kuwa, Marekani inataka kujitakasa na kuboresha muonekano wake machoni pa dunia kwa kutumia operesheni hiyo.
Zaidi ya magaidi 900 wakufurishaji wa Kiwahabi wa genge la Daesh (ISIS) wameangamizwa katika operesheni ya kuukomboa mji wa Mosul kutoka mikononi mwa kundi hilo, iiliyoanza Oktoba 19.
Haya yanajiri siku chache baada ya Waziri wa Ulinzi wa Iraq Khalid al-Ubaidi kusema nchi hiyo haihitaji ushiriki wa kijeshi wa Marekani kwa ajili ya kuukomboa mji wa Mosul. Amesisitiza kuwa, mwisho wa mwaka huu wa 2016 utakuwa pia ndio mwisho wa maisha ya kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh katika ardhi ya Iraq.
Mji huo ambao ulikaliwa kwa mabavu na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh hapo mwaka 2014, umeshuhudia mauaji makubwa ya maelfu ya vijana ambao walikataa kushirikiana na matakfiri hao wa Kiwahabi.