Feb 25, 2016 02:00 UTC
  • Al Azhar: Hakuna vita baina ya Shia na Suni nchini Syria

Licha ya njama zinazofanywa na Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel kwa ajili ya kuuhusisha mgogoro wa Syria na masuala ya kimadhehebu, Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri amesema kuwa vita vinavyoendelea nchini Syria si vita baina ya Shia na Suni.

Ahmad al Twatiib ambaye alikuwa akihutubia katika Kituo cha Utafiti wa Masuala ya Qur'ani mjini Jakarta huko Indonesia amesisitiza udharura wa kuungana nchi za Kiarabu na Kiislamu katika maslahi na malengo yao kwa ajili ya kufikia umoja na mashikamano kamili kati ya Waislamu na kusema kuwa, tofauti na madai yaliyotolewa na waziri wa vita wa Israel, Moshe Yaalun kuhusu mgogoro wa Syria, mgogoro huo si vita baina ya Shia na Suni.

Sheikh Mkuu wa al Azhar amesisitiza kuwa Waislamu wa madhehebu za Shia na Suni ni ndugu na kwamba hakukuwepo hitilafu na ugomvi baina na wafuasi wa madhehebu hizo katika historia. Sheikh Twayyib ametilia mkazo uharamu wa kuua Mwislamu sawa awe Shia au Suni na ametoa wito wa kurejea kwenye Uislamu na kupinga makundi yote yenye misimama ya kuchupa mipaka.

Matamshi hayo ya Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri yametolewa wakati Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel zikiendelea kupiga ngoma za vita nchini Syria na keneza propaganda za uongo kwamba mgogoro wa nchi hiyo ni vita baina ya Shia na Suni.

Tags