Hizbullah: Tuna matumaini ya kuwa na "Mashariki ya Kati Yenye Muqawama"
Sayyid Hashim Safiyyuddin, mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon amesema ushindi na kujitolea mhanga Ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu kutawezesha kujengwa mustakabali wenye kung'ara kwa Umma wa Kiislamu na kuanzishwa "Mashariki ya Kati Yenye Muqawama".
Mkuu wa Baraza la Utendaji la harakati ya Hizbullah ameeleza kuridhishwa na matokeo ya vita vya Syria, Iraq na Yemen pamoja na mabadiliko yote yaliyojiri katika Mashariki ya Kati na kueleza kwamba: "Eneo hili ambalo linategemea mataifa ya muqawama halitakuwa na nafasi kwa siasa za Marekani na vibaraka wake".
Sayyid Hashim Safiyyuddin ameashiria kuendelea kuwepo wanamuqawama wa Lebanon katika mstari wa mbele kwenye medani ya mapambano dhidi ya magaidi nchini Syria na kueleza kwamba muqawama uko katika hali bora kabisa kwa idadi ya wapiganaji, silaha na uwezo wa kijeshi na kisiasa ndani ya Lebanon na katika eneo.
Mkuu wa Baraza la Utendaji la Hizbullah ya Lebanon aidha ameeleza kufurahishwa na kuchaguliwa rais mpya wa nchi hiyo na kusisitiza kuwa kuna ulazima wa kufanyika jitihada za kuharakisha uundaji serikali kwa kushirikishwa Walebanon wote.
Itakumbukwa kuwa baada ya miaka miwili na nusu ya mkwamo wa kisiasa, tarehe 31 ya mwezi uliopita wa Oktoba, bunge la Lebanon lilimchagua Michel Aoun kuwa rais wa 13 wa nchi hiyo.
Baada ya kushika hatamu za uongozi, Rais Aoun alimteua Saad Hariri, kiongozi wa harakati ya Al-Mustaqbal kuwa Waziri Mkuu na kumpa jukumu la kuunda serikali.../