Nov 22, 2016 06:21 UTC
  • Magaidi washambulia msikiti kwa bomu na kuua makumi Kabul, Afghanistan

Makumi ya watu wameuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi lililolenga msikiti wa Kishia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul, wakati wa maadhimisho ya Arubaini ya Imam Hussein AS.

Fraidoon Obaidi, Mkuu wa Kitengo cha Upelelezi cha Polisi ya Kabul amesema kuwa, gaidi wa kujitolea muhanga alijiripua ndani ya Msikiti wa Baqir ul Olum mjini Kabul palipokuwa pakifanyika marasimu ya Arubaini ya Imam Hussein AS, mjukuu wa Mtume Muhammad SAW; na kuua watu wasiopungua 40, mbali na kujeruhi wengine 50 aghalabu yao wakiwa ni watoto wadogo.

Maafisa usalama nje ya msikiti ulioshambuliwa na magaidi Kabul

Wakati huo huo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bahram Qassemi amelaani hujuma hiyo ya kigaidi na kusema kuwa, karibuni hivi ugaidi utawatumbukia nyongo wafadhali na waungaji mkono wa harakati za kigaidi duniani. Sambamba na kutoa mkono wa pole kwa familia za wahanga wa hujuma hiyo, serikali na taifa la Afghanistan kwa jumla, Qassemi amesema ugaidi unaweza kutokomezwa katika eneo hili kupitia juhudi na ushirikiano wa jamii ya kimataifa.

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Bahram Qassemi

Itakumbukwa kuwa, Oktoba 10 na 11 wakati wa maadhimisho ya Tasua na Ashura, magaidi walishambulia Msikiti wa Char Yar ulioko katika eneo la Karte Char, viungani mwa mji wa Kabul pamoja na Haram ya Karte Sakhi katika mji huo na kuua makumi ya watu na kujeruhi wengine wengi.

Aidha mwezi Agosti mwaka huu, Waislamu wasiopungua 85 waliuawa na wengine zaidi ya 400 kujeruhiwa katika shambulizi la bomu lililofanywa na wanachama wa kundi la kigaidi la Daesh dhidi ya maandamano ya amani ya Waislamu wa madhehebu ya Shia katika mji mkuu wa Afghanistan, Kabul.

Tags