Wabahrain waandamana dhidi ya Waziri Mkuu wa Uingereza
Wananchi wa Bahrain wamefanya maandamano kueleza ghadhabu zao dhidi ya Waziri Mkuu wa Uingereza ambaye yuko nchini humo kushiriki mkutano wa kila mwaka wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi (P)GCC.
Maandamano makubwa yalishuhudiwa jana jioni katika kijiji cha Sitra, huku waandamanaji wakiikosoa serikali ya London kwa kuendelea kuunga mkono na kuukingia kifua utawala wa Manama, unaowakandamiza wananchi.
Hata hivyo, maandamano hayo yalitibuka baada ya maafisa usalama kutumia mabomu ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji hao.
Theresa May, Waziri Mkuu wa Uingereza aliwasili mjini Manama siku ya Jumatatu, kushiriki mkutano wa 37 wa kila mwaka wa (P)GCC na kupokewa na Waziri Mkuu wa Bahrain Mwanamfalme Khalifah bin Salman Al Khalifah.
Akizungumza mjini London kabla ya safari hiyo, May aliashiria kuwa hatozungumzia suala la ukandamizaji unaofanywa na utawala wa Aal-Khalifa, unaoendesha nchi hiyo ndogo ya Kiarabu kwa mkono wa chuma.
Ikumbukwe kuwa, Bahrain imekuwa ikishuhudia maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa Aal Khalifa tangu Februari mwaka 2011. Matakwa makuu ya wananchi hao ni kuwepo utawala wa kisheria, kukomeshwa ubaguzi wa kimadhehebu, kufanyika mageuzi ya kisiasa na kuheshimiwa haki za binadamu.
Maelfu ya wananchi wa Bahrain wanashikiliwa katika magereza na korokoro za nchi hiyo huku 150 kati yao wakiwa wamehukumiwa vifungo vya maisha jela. Hii ni licha ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kieneo na kimataifa kuendelea kulalamikia ukandamizaji huo na kuitaka serikali ya nchi hiyo iheshimu haki za raia wake.