Watu 24 wauawa kwenye miripuko miwili ya mabomu mjini Baghdad
Miripuko miwili ya mabomu iliyotokea leo Jumapili kwenye soko lenye shughuli nyingi katika mji mkuu wa Iraq, Baghdad, imepelekea watu 24 kuuawa na wengine 60 kujeruhiwa.
Miripuko hiyo imetokea kwenye wilaya ya Sadr yenye Waislamu wengi wa Kishia. Hakuna kundi lolote lililotangaza kuhusika na mashambulio hayo ya kigaidi ingawa mara nyingi genge la kitakfiri la Daesh ndilo hutangaza kuhusika na mashambulio kama hayo.
Polisi wanasema kuwa, kuna uwezekano idadi ya vifo ikaongezeka kutokana na kuwa hali za baadhi ya majeruhi ni mbaya.
Mashambulio hayo yamekuja huku habari zikisema kuwa, mapema leo Jumapili, kundi la kigaidi la Daesh limefanya mashambulizi makubwa katika viunga vya Baghdad.
Maafisa usalama wa Iraq wamesema kuwa, leo magaidi hao wamefanya mashambulizi makubwa katika eneo la Abu Ghraib, lililoko umbali wa kilomita 25, magharibi mwa Baghdad.