Dec 25, 2016 08:04 UTC
  • Mtikisiko wa kiuchumi waifanya Saudia ianze kuuza hisa za Aramco

Saudi Arabia imetangaza mpango wa kuanza kuuza karibu nusu ya hisa za shirika kubwa la mafuta nchini humo Aramco, ikiwa ni katika juhudi za kupunguza nakisi ya bajeti ya utawala huo.

Gazeti la Saudia la al-Eqtisadiah limeripoti kuwa, utawala wa Riyadh unapania kuuza asilimia 49 ya hisa za shirika hilo, ndani na nje ya nchi katika muda wa miaka 10 kuanzia mwaka 2018. Siku ya Akhamisi Saudia ilitabiri kuwa bajeti yake ya mwaka ujao itakuwa na nakisi ya dola bilioni 53 za Marekani.

Mkuu wa Aramco, Amin Nasser amesema kuanzia mwaka ujao shirika hilo litaanza kuchapisha matokeo yake baada ya kila miezi mitatu ili kuwavutia wawekezaji.

Shirika la Aramco la Saudia

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wanaitakidi kuwa, nakisi kubwa ya bajeti ya Saudi Arabia imetokana na uingiliaji kijeshi ufalme huo katika nchi jirani ya Yemen na pia kujiingiza katika masuala ya ndani ya nchi za eneo, mambo ambayo yamepelekea watawala wa ukoo wa Aal-Saud kujipata katika hali ngumu ya kiuchumi.

Mwezi Septemba mwaka huu, utawala wa Riyadh uliwafutia marupurupu wafanyakazi wa sekta za umma, sambamba na kupunguza mishahara ya mawaziri na wanachama wa Baraza la Shura kwa asilimia kati ya 15 na 20.

Mapema mwezi huu, Mfalme Salman Bin Abdul Aziz wa Saudia alisema ingawaje hatua hiyo ni chungu na itakayowasababishia wafanyakazi wa sekta za umma msongo wa mawazo, lakini Riyadh imelazimika kuandaa sera hizo ili kuunusuru uchumi wa nchi na kuzipatia ufumbuzi changamoto za kifedha zinazoikabili nchi hiyo.

 

Tags