Syria: Hatuna imani na watawala wa Uturuki
Ali Abdul Karim Ali, balozi wa Syria nchini Lebanon amesema, Damascus haina imani na watawala wa hivi sasa wa Uturuki kwani Ankara ndiyo nguzo kuu ya uungaji mkono wa kifedha na kifikra kwa ugaidi ulioenea leo hii kwenye eneo hili.
Mgogoro wa Syria ni medani ya kutathminiwa kiwango cha welewa wa nchi za eneo hili hususan madola ya Mashariki ya Kati, katika upande wa kisiasa na kiusalama, na vile vile taathira za kuenea machafuko na ukosefu wa amani kwa usalama wa madola hayo. Baada ya kupita takriban miaka sita tangu kutumbukizwa Syria kwenye mgogoro, hivi sasa tunaweza kutoa tathmini ya kina zaidi kuhusu siasa za madola ya eneo hili ikiwemo Uturuki. Kabla ya kuanza maandamano dhidi ya tawala za ulimwengu wa Kiarabu mwaka 2011, Uturuki ilifuata siasa za kujiepusha kikamilifu kuwa na migogoro na majirani zake, na siasa hizo zilijikita kwenye kuimarisha uhusiano wake na majirani zake hususan Syria. Kabla ya mwaka 2011, hakukuwa na mgogoro unaohisika baina ya Uturuki na majirani zake ikiwemo Syria.
Hata hivyo, kama zilivyofanya nchi nyingine za eneo hili, serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki, ilishindwa kuwa na tathmini nzuri kuhusiana na malalamiko dhidi ya tawala za ulimwengu wa Kiarabu yaliyoanza mwaka 2011 hususan yale ya nchini Syria. Uturuki pamoja na baadhi ya nchi za Kiarabu hususan Saudi Arabia zilifuata kibubusa siasa za madola ya Magharibi kama vile Marekani, Ufaransa na Uingereza za kutaka kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria. Serikali ya Uturuki ilikuwa mwenyeji wa vikao vingi sana vya wapinzani wa utawala wa Syria. Baya zaidi ni kwamba Uturuki ilifungua mipaka yake kwa ajili ya magaidi kuingia na silaha nzito nzito ndani ya Syria na kuanza kufanya jinai dhidi ya wananchi na maafisa wa serikali ya Damascus. Matokeo ya siasa mbovu za Uturuki kuhusu mgogoro wa Syria ni kwamba, si tu zimeshindwa kufikia malengo yake ya kuipindua serikali ya Rais Bashar al Assad, lakini pia zimepelekea Uturuki ikumbwe na mgogoro mkubwa usalama na kila leo kunashuhudiwa mashambulizi ya kigaidi katika kona mbalimbali za nchi hiyo suala ambalo limeathiri moja kwa moja uchumi wa Uturuki na sekta zake hususan ile ya utalii.
Mapinduzi yaliyofeli ya mwezi Julai 2016 nchini Uturuki, yalifungua macho ya watawala wa Uturuki kuhusiana na nani ni rafiki na nani ni adui yao. Kinyume kabisa na madola ya Magharibi na baadhi ya nchi za Kiarabu ambazo zilichelewa kuonesha radiamali zao, Russia na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran zilikuwa nchi za kwanza kabisa zilizolaani haraka sana jaribio hilo la mapinduzi ya kijeshi. Misimamo ya wazi na ya haraka sana ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Russia ya kulaani jaribio la kuipindua serikali ya Uturuki iliifanya serikali ya Ordogan ibadilishe msimamo wake kuhusiana na utawala wa Syria. Ijapokuwa hadi hivi sasa Uturuki inapiga domo la kuipinga serikali ya Rais Bashar al Assad wa Syria, lakini upinzani huo unaonekana wazi kuwa umepungua mno makali yake. Msimamo huo mpya wa serikali ya Uturuki umebadilisha pia misamiati ya matamshi ya viongozi wa Syria. Sambamba na kuashiria namna misimamo ya viongozi wa Uturuki ilivyobadilika kuhusiana na Syria, Balozi Ali Abdul Karim Ali wa nchi hiyo huko Lebanon amesema, hivi sasa Uturuki haina njia nyingine ila kubadilisha misimamo yake kuhusiana na serikali ya Rais Bashar al Assad baada ya kuona njama zake na za madola ya Magharibi hususan Marekani zimeshindwa, na magenge ya kigaidi yanazidi kusambaratishwa. Na ndio maana pia viongozi wa Uturuki wamelazimika kushiriki kwenye mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Syria huku wakisisitizia wajibu wa kulindwa umoja wa ardhi nzima ya nchi hiyo.
Kuna na masuala mengine katika misimamo ya serikali ya Ankara ambayo yanawafanya viongozi wa Syria wasiwe na imani na watawala wa Uturuki. Miongoni mwa misimamo hiyo ni sisitizo la serikali ya Ordogan la kuondoka wanamapambano wa Hizbullah nchini Syria. Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameijibu serikali ya Ankara kwa kusema, kinyume kabisa na magenge ya kigaidi yaliyoivamia ardhi ya Syria kupitia Uturuki, Hizbullah ya Lebanon iko nchini Syria kwa ombi rasmi la serikali halali ya nchi hiyo, hivyo, kitendo cha Uturuki cha kutaka Hizbullah iondoke nchini Syria ni ombi lisilo na maana hata kidogo.